Ujerumani imesisitiza kwamba ndiyo inayowajibika kwa mauaji ya Wayahudi wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Hii ni baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuibua mzozo mkubwa baada yake kudai kiongozi mmoja wa Wapalestina ndiye aliyewaambia viongozi wa chama cha Nazi kuwaua Wayahudi barani Ulaya.
Chansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema Wajerumani wanafahamu wazi kwamba viongozi wa Nazi ndio waliopanga na kutekeleza mauaji hayo yajulikanayo kama Holocaust.
Netanyahu alikuwa amedai kiongozi wa Nazi Adolf Hitler alitaka tu kuwafurusha Wayahudi kutoka Ulaya, lakini Mufti Mkuu wa Jerusalem Haj Amin al-Husseini akamwambia: "Wachome moto."
Matamashi hayo yamekashifiwa vikali na wanahistoria wa Israel pamoja na wanasiasa.
Akiongea kando ya Merkel mjini Berlin, Bw Netanyahu alikuwa awali amesema "hakuna anayefaa kukana kwamba Hitler aliwajibika kwa kutekeleza mauaji ya Wayahudi".
Lakini Jumanne katika hotuba ya Baraza Kuu la Wazayuni Duniani mjini Jerusalem, Bw Netanyahu alidai Husseini ndiye aliyetoa wazo la kuwaangamiza Wayahudi.
"Hitler hakutaka kuwaangamiza Wayahudi wakati huo – alitaka tu kuwafurusha,” aliambia kongamano hilo.
"Na Haj Amin al-Husseini alimwendea Hitler na kusema: 'Ukuwafurusha, wote watakuja hapa.’
“’Basi nifanye nini nao?’ [Hitler] alimwuliza. Yeye [Husseini] akamjibu: ‘Wachome moto.'"
BBC
No comments:
Post a Comment