Shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka, Damian Chilumba, katika kesi ndani ya kesi iliyoibuka wakati wa usikilizwaji wa kesi ya mauaji ya kukusudia ya mfanyabiashara, bilionea wa madini ya Tanzanite, Erasto Msuya (43), amedai mshtakiwa Mussa Mangu, ndiye aliyeisaidia Polisi kumtia mbaroni ‘bosi’ aliyesuka mpango mzima wa mauaji hayo.
Chilumba ambaye kwa sasa ni Mkaguzi wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, alimedai baada ya kumkamata Mussa, aliwaeleza kwamba yeye binafsi hakushiriki mauaji hayo lakini mipango yote ya mauaji ilisukwa na bosi wake anayeitwa Sharif Athuman.
Kesi hiyo ndani ya kesi (Trial within Trial) ilianza wiki iliyopita baada ya Wakili Emanuel Safari anayemtetea mshtakiwa wa tatu, kuibua hoja kwamba, mshtakiwa Mussa Mangu aliteswa kiakili ikiwamo kupokea kipigo kilichosababisha akaumizwa puani wakati wa kumhoji na kumshinikiza kuandika maelezo yake ili ayasaini kwamba amekiri kosa.
Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi Agosti 7, mwaka 2013, majira ya saa 6:30 mchana katika eneo la Mijohoroni, kando ya barabara kuu ya Arusha-Moshi, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia).
Shahidi huyo akiwa mbele ya Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo, alidai baada ya kuelezwa hivyo, alimuuliza mshtakiwa huyo bosi wake anapatikana wapi kwa muda huo na kujibu kuwa Sharif ana nyumba nyingi lakini siku hiyo saa tano usiku alikuwa amemuaga kwamba anaelekea nyumbani kwake Tengeru.
Sehemu ya mahojiano kati ya Wakili Mkuu wa Serikali, Neema Mwenda na shahidi huyo yalikuwa hivi:
Wakili Neema: Shahidi wakati mmefika nyumbani kwa mshtakiwa kumkamata, upekuzi wenu ulikuwaje?.
Shahidi: Kwa sababu tulikuwa hatujakamata bunduki iliyotumika katika mauaji ya Msuya, tulimpekua Mussa nyumbani kwake ili kutafuta simu iliyotumika kufanya mawasiliano, risasi na pikipiki ambayo ilitumika katika tukio hilo.
Wakili Neema: Shahidi baada ya hapo mlipata nini?.
Shahidi: Hatukupata chochote lakini tukiwa tunaendelea kumpekua, mshtakiwa alisema kuna kitu anataka aongee, nikamwambia asubiri kwanza ataniambia baadae.
Wakili Neema: Na baada ya kumaliza kumpekua, mshtakiwa alikueleza nini alichotaka kukuambia awali?
Shahidi: Alidai kwamba yeye binafsi hajashiriki katika kosa analotuhumiwa nalo ila mauaji hayo yalipangwa na bosi wake aliyemtaja kwa jina moja la Sharrif. Tukamuuliza anapatikana wapi kwa muda huo, akajibu Sharif ana makazi mengi lakini majira ya saa tano za usiku alimuaga anakwenda Tengeru, nikaona hiyo ni habari muhimu kwetu, ndo tukaanzia hapo.
Wakili Neema: Shahidi hebu ieleze mahakama, baada ya taarifa hiyo unayosema ilikuwa muhimu kwenu, nini kilifuata?.
Shahidi: Nilimuarifu RCO wangu wa Kilimanjaro, Ramadhan Ng’anzi (Mkuu wa Upelelezi Mkoa) kuhusu taarifa hiyo mpya na akanielekeza twende hadi aliko mshtakiwa mwingine tukamkamate.
Wakili Neema: Baada ya kufika Tengeru nini kilitokea?
Shahidi: Mshitakiwa Mussa Mangu alianza kusita sita huku akitueleza kwamba hapajui vizuri kwa bosi wake huyo, lakini ghafla tena akatushauri turudi kule tulipomkamatia, kwa sababu karibu na nyumbani kwake, kuna makazi mengine ya bosi wake. Hapo tukagundua anatudanganya.
Wakili Neema: Kwa nini alianza kusita sita kuwaonyesha alipo huyo aliyemtaja ni bosi wake?.
Shahidi: Hiyo ndiyo tabia ya wahalifu ili akufikishe kwa mwenzake ni lazima akusumbue sana.
Wakili Neema: Sasa baada ya kumkosa mshitakiwa ambaye ni bosi wake, mlirudi saa ngapi kwenye ngome yenu alipokuwa RCO?.
Shahidi: Siwezi nikasema ni muda gani exactly (muda sahihi) lakini ni kati ya saa 10 na saa 10:15 alfajiri.
Wakili Neema: Shahidi hebu isaidie mahakama, wakati unakwenda kumkabidhi mshtakiwa kwa RCO mlikuwa armed (mlikuwa na silaha)?.
Shahidi: Ndio, Koplo Atwaibu ndiye aliyekuwa na silaha peke yake.
Baada ya mahojiano hayo, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Hudson Ndusyepo ulianza kumhoji Inspekta Damian Chilumba kama ifuatavyo:
Wakili Hudson: Labda shahidi utusaidie, umesema mlifanya searching (upekuzi) wa dharura. Je, ni wakati gani mlifanya searching na wakati gani mlimhoji mshtakiwa Mussa?
Shahidi: Wakati tunafanya upekuzi na yeye Mussa alikuwapo na ndiko alikotueleza hakushiriki tukio la mauaji ila anamfahamu aliyepanga kutekeleza mauaji ya Msuya.
Wakili Hudson: Mlipofika Tengeru na mshtakiwa akaanza kuwababaisha, mlienda wapi?.
Shahidi: Mshtakiwa (Mussa) alitoa plani B, akitaka turudi tulipomkamatia kwa sababu bosi wake ana makazi mengi na alikuwa ana makazi mengine karibu na nyumbani kwake.
Wakili Safari: Hebu tusaidie shahidi, search ilichukua muda gani?.
Shahidi: Ilichukua saa mbili na dakika 20 hivi.
Wakili Safari: Kutoka saa 7 usiku, ukiongeza saa nyngine mbili unapata saa ngapi?
Shahidi: Saa tisa.
Wakili Safari: Hivi wakati mnafanya upekuzi mlikuwa na kibali chochote toka kwa OC-CID wa Arusha?.
Shahidi: Ndio, nilikuwa na kibali cha emergence (dharura) ila sikukijaza kwa sababu sikuona umuhimu.
Muda mfupi baadae mahakama hiyo ilitoa fursa kwa upande wa utetezi nao kuita mashahidi wao kwa ajili ya kutoa ushahidi katika kesi ndani ya kesi na shahidi wa kwanza, Mussa Mangu ambaye ni mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo ya mauaji ya bilionea Msuya, utetezi wake ulikuwa hivi:
Wakili Safari: Shahidi unaweza kuiambia mahakama hii ni kwa nini upo gerezani?
Shahidi: Nimeshtakiwa kwa kosa la mauaji ya Erasto Msuya.
Wakili Safari: Unakumbuka ulikamatwa lini na akina nani?.
Shahidi: Nilikamatwa tarehe 11/8/2003 na askari polisi nyumbani kwangu Shangarai-Kwa Mrefu nikiwa nimepumzika na familia yangu.
Wakili Safari: Shahidi kule polisi waliposimamisha gari lao baada ya kukukamata na kukufungua kitambaa walichokuwa wamekufunga machoni unapakumbuka?.
Shahidi: Siwezi kupakumbuka kwa sababu kulikuwa porini ila namkumbuka shahidi aliyeondoka hapa Inspekta Chilumba ndiye aliyetoa amri nipigwe ili niseme nilivyohusika katika mauaji ya Erasto Msuya.
Wakili Safari: Hebu tusaidie, baada ya kutolewa pale kwa RCO wa Arusha, ulipelekwa wapi?.
Shahidi: Nilipelekwa Kituo cha Polisi cha Kisongo ambacho polisi wanakiita Guantanamo-kituo cha mauaji na baadae wakanipeleka katika Gereza la Kisongo.
Wakili Safari: Baada ya kufika huko ikawaje?.
Shahidi: RCO (Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa) alitoa amri nipigwe na askari wake wakatekeleza amari hiyo.
Wakili Safari: Walikufanyaje ukiwa huko Guantanamo ya Kisongo?.
Shahidi: Walinifunga unyayo na kunipiga kwa bomba la chuma, wakanivua suruali na kuchukua spoku ya baiskeli na kuingiza ndani ya uume wangu wakiniambia nieleze jinsi tukio zima la mauaji lilivyopangwa na lilivyotekelezwa.
Wakili Safari: Unakumbuka ulipotolewa Arusha huko Guantanamo ulipelekwa wapi?
Shahidi: Nililetwa Moshi lakini kabla ya hapo nilipelekwa Kituo cha Polisi Kia.
Wakili Safari: Sasa ulipelekwa lini Moshi mjini?.
Shahidi: Tarehe 21/8/2013 ndio nililetwa Moshi Central (Kituo Kikuu cha Polisi).
Upande wa mashtaka katika kesi hiyo unaongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Neema Mwenda akisaidiwa na mawakili waandamizi watatu, Abdallah Chavula, Stella Majaliwa na Baraka Nyambita.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment