Polisi mkoani Shinyanga imewaonya wafuasi wa vyama vya siasa ambao wamekuwa wakijitangazia ushindi mapema kabla ya uchaguzi kufanyika, hali ambayo imekuwa ikionyesha kuwapo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani siku ya kupiga kura endapo matarajio yao ya matokeo yakakwenda tofauti.
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Justus Kamugisha, alitoa onyo hilo katika kikao cha wadau cha kujadili namna ya kudumisha amani siku ya uchaguzi Oktoba 25, mwaka huu kilichoandaliwa na shirika la Save the children mkoani hapa.
Kamugisha alisema anasikitishwa na baadhi ya wafuasi wa vyama vya siasa kuanza kujitangazia ushindi mapema kwa wagombea wao kuwa wao ndiyo wameibuka kidedea hata kabla upigaji kura kutofanyika, kitendo ambacho aliomba kikome.
“Ndugu zangu, amani ya nchi hii ipo mikononi mwa Watanzania wenyewe, hivyo ni vyema wakafanya uchaguzi kwa amani na kutii sheria bila shuruti, kusiwapo na vurugu za aina yoyote, polisi tumejipanga kwa asilimia 100 kwa yeyote atakayekiuka sheria lazima tumuadhibu,” alisema Kamanda Kamugisha.
Hata hivyo, Kamugisha aliwaasa viongozi wa vyama hivyo vya siasa na asasi za kiraia zielekeze nguvu zaidi kutoa elimu ya upigaji kura, kuhesabu na kutangazwa kwa matokeo kwa muda huu mchache uliosalia ili wananchi wafahamu ni mtu gani anayestahili kutangaza matokeo ya uchaguzi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Allynasoro Rufunga, akizungumza katika kikao hicho, alilaani kusikia baadhi ya wafuasi wa vyama vya siasa wamepanga kufanya vurugu siku ya uchaguzi endapo matarajio yao ya matokeo yatakwenda tofauti na kuwaasa wakumbuke kuna maisha mara baada ya uchaguzi.
No comments:
Post a Comment