Wednesday 28 October 2015

POLISI WAONJA MACHUNGU YA MAJI YAKUWASHA!


NB-Siyo gari la polisi lililosababisha majanga

Polisi wanne waliokuwa doria wakati wa uchaguzi juzi usiku, walijikuta wakionja machungu ya maji ya kuwasha, baada ya kumwagiwa na wenzao wakati wakijaribu kuwatawanya wafuasi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) waliokuwa wakisherehekea matokeo ya udiwani. 




Kufuatia tukio hilo katika Kata ya Makumbusho, Dar es Salaam, askari hao walijikuta mikononi mwa raia wakipatiwa msaada wa huduma ya kwanza kutokana na gari lao kumwagiwa maji ya kuwasha, kufuatia gari lililokuwa mbele yao kufyatuka pampu na kuanza kurusha maji hayo.

Tukio hilo lilitokea katika Mtaa wa Mwananyamala A, karibu na nyumba za makazi ya watu, wakati magari matano ya askari yakiwa nyuma ya gari lenye maji ya kuwasha, wakijaribu kutuliza ghasia za wananchi waliokuwa wakiandamana kushangilia ushindi wa diwani aliyeshinda, Harub Ally.

Wakizungumza na Nipashe, wananchi hao walisema tukio hilo lilitokea wakati polisi hao wakijaribu kurusha maji hayo ili kuwatawanya, lakini pampu hiyo ilifyatuka na kuwamwagikia askari wenzao.

Kufuatia tukio hilo, wananchi walianza kuwapa msaada wa mafuta ya kujipaka na maji kabla ya kuelekea hospitali.

“Hawa askari walikuwa wanatumwagia haya maji ili kutuliza ghasia, lakini jambo la ajabu maji yakawamwagikia wao. Ilibidi tuwe wema tuanze kuwasaidia kwani hali zao zingekuwa mbaya sana na kama siyo msaada wetu raia wangedhurika sana,” alisema Haroub Juma. 

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!