Sunday, 4 October 2015

MSANII WA NYIMBO ZA ASILI MKOANI MWANZA AHUKUMIWA MIAKA 10 JELA KWA KUMILIKI FISI WAWILI BILA KIBALI

MAHAKAMA ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza, imemhukumu msanii wa ngoma za asili, Mng’ahwa Kazanza (42), kwenda jela miaka 10 kwa kosa la kumiliki fisi wawili na kuwatumia kwenye sanaa zake bila kibali. 

Awali akisomewa mashtaka katika mahakama hiyo na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Doroth Mgenyi, ilielezwa mahakamani hapo kuwa mnamo Septemba 28, mwaka huu, kwenye Kijiji cha Sisu wilayani Misungwi, majira ya saa 7:30 mchana, Mng’ahwa Kazanza (42) alikamatwa akiwa na fisi wawili wenye thamani ya Sh milioni 4.8. 
Mara baada ya kusomewa mashtaka, msanii huyo alikiri kosa hilo na kudai alikuwa akiwatumia fisi hao katika sanaa zake bila kutambua kama ni kosa kuburudisha mashabiki wake kwa lengo la kuongeza kipato. 
Kutokana na kukiri huko, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ruth Mkisi, alimtia hatiani kwa kosa la kupatikana na nyara za Serikali kinyume cha sheria Na. 5 ya mwaka 2009 na kumhukumu kwenda jela miaka 10 au kulipa faini ya Sh 4,840,000 ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaomiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria. 
Msanii huyo alishindwa kulipa faini hiyo na hivyo kwenda jela kutumikia adhabu hiyo ya miaka 10.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!