Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, amesema Dola za Marekani milioni 409, zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa mfumo wa kuondoa maji ya mafuriko na majitaka Dar es Salaam, ili wakazi wa jiji hilo waweze kuishi kuwa ustaarabu.
Pia alisema fedha hizo zitatumika kujenga mfumo wa kutibu maji taka yatakayotumika kwa shughuli zingine badala ya kuyaacha yakimwagika baharini.
Alisema hayo jijiji hapa jana katika hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa).
Alisema fedha hizo ni msaada kutoka Benki ya Dunia ambayo imewapatia Dola za Marekani milioni 220, Serikali ya Korea Kusini imetoa dola milioni 89 na Serikali ya Tanzania kwa upande wake imetoa dola milioni 100.
“Dar es Salaam, mvua ikinyesha mfumo mzima wa majitaka unakuwa sehemu ya mafuriko, hii inaleta adha kubwa kwa wakazi wa jiji hilo…kwa hiyo ni lazima bodi isimamie ujenzi mzuri wa mifumo hiyo ili jiji liwe la kistaarabu kwa kuishi,” alisema.
Aidha, alisema chini ya mpango huo, serikali itahakikisha kila mtu anakuwa na maji nyumbani kwake.
Akizungumzia makusanyo ya mapato, alisema kwa sasa mapato ya Dawasa na Dawasco yameongezeka kutoka Sh. bilioni 2.6 hadi kufikia Sh. bilioni 4.2.
Hata hivyo, alisema baada ya mfumo wa maji kuimarika mapato hayo yanatakiwa kuongezeka na kufikia makusanyo ya Sh. bilioni 11.
Aliwataka wajumbe hao kufanya kazi kwa juhudi kubwa kuhakikisha maji yanapatikana hususan katika miji yote mikubwa kusiwe na tatizo hilo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Dawasa, Dk. Eve Hawa Sinare, alisema bodi yake inakamilisha miradi mikubwa yote na kumpongeza Waziri Maghembe kwa kutoingilia shughuli za utendaji wa bodi hiyo.
Chini ya mabadiliko ya muundo wa bodi, Mwenyekiti wa Dawasa sasa anakuwa mjumbe katika Bodi ya Dawasco, na Mwenyekiti wa Dawasco pia anakuwa mjumbe katika Bodi ya Dawasa kwa lengo la kuleta ufanisi.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mbogo Futakamba, alisema wizara hiyo inataka kuhakikisha jiji la Dar es Salaam linapata maji safi muda wote.
No comments:
Post a Comment