Wednesday, 21 October 2015

MAGUFULI KUUNGURUMA DAR SIKU 3

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli akihutubia maelfu ya wakazi wa Sengerema mkoani Mwanza wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Mnadani jana. (Picha na Adam Mzee).

MGOMBEA wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli leo anaanza kampeni katika mkoa wa Dar es Salaam, ambako atanguruma kwa siku tatu. Atafanya kampeni Dar, baada ya kutikisa katika mikoa ya Mwanza na Geita. Jana, Dk Magufuli alikuwa na mikutano katika baadhi ya majimbo ya Geita.


Kisha aliendelea mkoani Mwanza, ambapo jana alasiri alinguruma katika mji wa Sengerema, ambao aliwahi kuishi, akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati katika shule ya sekondari ya Sengerema mwaka 1981.
Kwa mujibu wa Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba “Gaddafi’, Dk Magufuli ataanza kampeni katika Jimbo la Kigamboni kuanzia saa mbili asubuhi, katika mkutano utakaofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Machava.
Baada ya mkutano huo, mgombea huyo wa CCM ambaye ametamba kuwa ana nafasi kubwa ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano ya Tanzania, atakwenda Jimbo la Mbagala katika mkutano utakaofanyika eneo la Vigaeni Pub, Mbagala Zakhem.
“Baada ya mkutano wa Mbagala Zakhem, mgombea wetu atakwenda TMK (Temeke), katika mkutano utakaofanyika kwenye uwanja wa nyumbani, Mwembeyanga kuanzia saa sita mchana,” alifafanua Simba.
Aliongeza kuwa baada ya mkutano huo, Dk Magufuli ataenda Jimbo la Ubungo ambako atafanya mkutano kwenye uwanja wa michezo wa TP Uzuri, Sinza. Alisema Dk Magufuli atakamilisha mikutano yake mitano ya siku ya kwanza leo, kwa kufanya mkutano mwingine mkubwa kwenye Viwanja vya Biafra Jimbo la Kinondoni kuanzia saa 10 hadi 12 jioni.
Kesho Alhamisi, Dk Magufuli atakuwa na mikutano miwili mkoani Dar es Salaam, ambako asubuhi kuanzia saa tatu atakuwa katika Jimbo la Kibamba katika mkutano utakaofanyika Mbezi kwa Beda.
Saa 10 jioni hadi saa 12 atahutubia Jimbo la Kawe katika mkutano utakaofanyika Bunju shuleni. Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam alisema baada ya mkutano wa Jimbo la Kibamba, Dk Magufuli atakwenda mkoani Pwani kuendelea na kampeni, kabla ya kurejea jioni na kwenda kuhutubia Bunju jimboni Kawe.
“Tarehe 23 (Ijumaa) Dk Magufuli atakuwa na mkutano mkubwa katika Viwanja vya Jangwani kuanzia saa tano hadi saa kumi na mbili jioni. Tunawaomba wanachama wa CCM, wapenzi, mashabiki na wenye kuitakia mema nchi yetu, kujitokeza kwa wingi katika sehemu zote atakazokuwapo Dk Magufuli,” alisema Simba, aliyebainisha kuwa Jumamosi CCM Mkoa wa Dar es Salaam itahitimisha kampeni kwenye Viwanja vya Tanganyika Packers.
Tayari Dk Magufuli alikwishafanya mikutano katika majimbo ya Segerea na Ukonga wiki iliyopita. Mkutano wa Sengerema Akiwa Sengerema jana, Dk Magufuli alisema kama watu wangepata fursa ya kuufungua moyo wake, wangejionea ni jinsi gani alivyo na nia ya dhati ya kuwatumikia Watanzania, na ni kama anajitolea sadaka kuwatumikia.
Alisema anataka kwa dhati ya moyo wake, kuwatumikia Watanzania, na kwamba kwake muhimu ni maslahi ya Tanzania na siyo ya dini, kabila, rangi wala chama, kwani wananchi wote wanahitaji maendeleo.
“Nataka kuleta mabadiliko ya maisha, nitabaki na deni kwenu, nitaongoza bila kubagua vyama. Kwangu mimi kwanza ni kazi tu, sitaangalia maslahi ya vyama, dini, kabila, kwangu maslahi ni ya Tanzania.
Mimi ndiye ninayefaa kuongoza Tanzania mpya,” alisema Dk Magufuli. Aliwaahidi wananchi wa Sengerema kuwa hatawasahau, endapo atashinda uchaguzi wa Jumapili. Alisisitiza suala la amani, akisema wanasiasa wanaohubiri uchochezi, wakisema nchi itachimbika, hawaitakii mema Tanzania na wanapaswa kuepuka.
Aliwataka wananchi na hasa vijana, kujihadhari nao, kwani wakati watakapokumbana na mkono wa dola, wao watakuwa majumbani mwao. “Msidanganyike, mjihadhari na wanasiasa wanaohubiri chuki na uchochezi.
Amani ikivurugika vijana hamtaweza kuuza jojo zenu, hamtaendesha bodaboda, hamtauza soda, kama mna nyumba zenu nzuri mtazikimbia. Kuweni makini na wanasiasa wanaotaka kuwatumia kuandamana wakati wao watakuwa hawapo,” alionya.
Aliahidi kusimamia ufufuaji wa kilimo cha pamba, kulinda watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) na kuboresha miundombinu ya barabara. Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Sengerema, William Ngeleja alisema kujitokeza kwa wingi kwa wananchi wa Sengerema ni kutokana na imani kubwa kwao kwa Dk Magufuli, na pia imani kubwa kwa CCM baada ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010-2015 kwa mafanikio makubwa.
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, Abdallah Bulembo alisema Dk Magufuli hadaiwi na mtu, siyo mwizi au fisadi na kwamba chama hicho kimeteua mtu anayejiuza, hivyo wananchi wa Sengerema na Tanzania kwa ujumla, hawapaswi kufanya makosa ya kutomchagua kuwa Rais wao.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!