Thursday, 8 October 2015

MABISHANO YAZUKA JUU YA KESI YA BILIONEA ERASTO MSUYA


Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, imeipokea ripoti ya uchunguzi wa kifo cha mfanyabiashara bilionea wa madini ya Tanzanite, Erasto Msuya (43), iliyosainiwa  na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai, Dk. Paul Chaote, kama kielelezo muhimu, baada ya kuibuka mabishano makali ya kisheria kati ya jopo la mawakili wa utetezi na wa upande wa mashtaka.



 
Msuya aliuawa Agosti 7, mwaka 2013, saa 6:30 mchana katika eneo la Mijohoroni, kando kando ya barabara kuu ya Arusha-Moshi, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia).
 
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Sharif Athuman (31), ambaye ni mchimbaji mdogo wa madini na mkazi wa Kimandolu, mkoani Arusha, Shaibu Saidi maarufu Mredii (38), mkazi wa Songambele, wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara na Mussa Mangu (30), mkazi wa Shangarai kwa Mrefu.
 
Wengine ni Jalila Said (28), mkazi wa Babati, Sadiki Jabir maarufu Msudani (32), mkazi wa Dar es Salaam na Lang’ata, wilaya ya Hai, Karim Kihundwa (33), mkazi wa Lawate, wilaya ya Siha na Alli Musa maarufu Mjeshi, mkazi wa Babati, mkoani Manyara.
 
Kielelezo hicho kilipokelewa mahakamani hapo jana, baada ya shahidi wanne, Dk. Paul Chaote, aliyeufanyia uchunguzi wa kitabibu mwili wa Msuya kumaliza kutoa ushahidi wake mbele ya Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo ya mauaji ya kukusudia.
 
Hata hivyo, Wakili Majura Magafu anayewatetea washtakiwa wa pili na watano, alisimama na kutoa pingamizi la kisheria, akidai ripoti hiyo ilikuwa na mapungufu ya mahitaji ya kisheria ambayo ni kutoambatanishwa fomu namba 99 ya polisi na kwamba fomu hiyo haikuwa na jina kamili la mkuu wa polisi wa wilaya aliyetoa idhini ya kufanyika kwa uchunguzi huo.
 
Upande wa mashitaka unaongozwa na jopo la mawakili watatu waandamizi ambao ni Abdallah Chavula, Stella Majaliwa na Baraka Nyabita.
 
Baada ya kutolewa pingamizi hilo, Wakili Chavula alisimama na kujibu hoja hiyo kwamba kifungu cha 291 cha Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA) kimeweka utaratibu wa uandishi na upokeaji wa fomu za kitabibu na kwamba shauri lililopo mbele ya mahakama hiyo siyo Inquest (uchunguzi wa kifo chenye mashaka) bali ni mauaji.
 
Jaji Maghimbi aliingilia kati na kutoa mwongozo:  “Mahakama imeipokea ripoti hiyo ya uchunguzi wa kifo kama kielelezo, baada ya shahidi wanne kutoa ushahidi wake na kukidhi mahitaji ya kisheria.”
 
MASHAHIDI WATATU HAWAKUTOKEA 
Hata hivyo, mahakama hiyo jana ililazimika kuahirisha shughuli zake kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo hadi leo, baada ya mashahidi watatu wa upande wa mashtaka kushindwa kufika mahakamani, wakidaiwa kuwa safarini.
Wakili Chavula, akiwa mbele ya Jaji Salma Maghimbi alidai mashahidi hao waliokuwa watoe ushahidi wao, wameshindwa kufika mahakamani kwa kuwa wapo safarini wakitokea nje ya mkoa kwenda Moshi.
 
“Mheshimiwa Jaji leo (jana) tumejiandaa kuwa na mashahidi watatu ambao wanatoka nje ya mkoa wa Kilimanjaro. 
 
Kwa bahati mbaya mpaka hivi sasa hawajafika na hatuna shahidi mwingine wa kuendelea nae siku ya leo…mtukufu Jaji, tunaiomba mahakama yako itoe ahirisho mpaka siku ya kesho (leo) kama wenzetu wa utetezi hawatakuwa na pingamizi,” aliomba  Wakili Chavula.
 
Baada ya maelezo hayo, kiongozi wa jopo la mawakili wa upande wa utetezi, John Lundu, alisimama na kueleza hawana pingamizi kuhusu ombi hilo la upande wa mashtaka, isipokuwa wanaiomba mahakama itoe amri mashahidi hao wafike mahakamani kwa wakati ili watoe ushahidi wao.
 
Jaji Maghimbi alikubaliana na hoja za pande zote mbili na kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba  8, mwaka huu, mahakama itakapoendelea na usikilizwaji wa shauri hilo namba 12 la mwaka 2014.
 
Juzi shahidi wa nne katika kesi hiyo, Dk. Paul Chaote ambaye alikuwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai (DMO), aliieleza mahakama hiyo kwamba alipoufanyia uchunguzi wa kitabibu mwili wa mfanyabiashara huyo, aliukuta ukiwa na majeraha 26 yaliyotokana na risasi.
 
Alidai majeraha aliyoyagundua katika mwili wa marehemu Msuya, makubwa yalikuwa 13 na madogo 13 ambayo kitaalam yalionyesha yametokana na risasi zilizopigwa umbali mfupi.
 
 “Nilipouchunguza nilikuta damu nyingi zikivuja puani, masikioni na mdomoni. Kichwani kulikuwa na jeraha kubwa na nyuma ya kichwa ubongo ulikuwa ukining’inia…Kulikuwa pia na jeraha kwenye paji la uso na pembeni yake,” aidai na kuongeza: 
 
“Lakini pia kulikuwa na jeraha kwenye bega na nyuma ya uti wa mgongo kwenye mbavu ya tano na ya sita kulikuwa na jeraha moja. Jeraha jingine lilikuwa chini ya kitovu na juu ya tumbo. Kwa ujumla majeraha hayo yote yalikuwa yamesababishwa na kitu chenye ncha kali kinachotembea mwilini kwa kasi. Ukubwa wa jeraha dogo lilikuwa ni kati ya sentimita moja na nusu hadi tano na makubwa sentimita nane.”
 
Naye shahidi wa tatu katika kesi hiyo, Raphael Karoli (58), mkazi wa kijiji cha Embukoi, wilaya ya Siha na mfugaji wa jamii ya Kimasai, alieleza mahakama hiyo kwamba, siku mauaji hayo yanafanywa  alikuwa nyumbani kwake na wafugaji wengine takribani 10 na aliwaona watu wawili wakiwa na pikipiki iliyopata pancha tairi la mbele na aliwaamuru wenzake kuwafuata na kuwazuia ili kujua ni akina nani lakini walitelekeza pikipiki na kukimbilia korongoni ambako ng’ombe wao hunywa maji mchana.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!