Tuesday, 6 October 2015

HUJAJI MWINGINE ABAINIKA KUFA MAKKAH NCHINI SAUDI AERABIA


Hujaji mwingine wa Tanzania, Khamis Juma Shamte, amegundulika kuwa amekufa katika tukio la mkanyagano wa mahujaji lililotokea  Septemba 24, mwaka huu, eneo   la Mina, Makkah, nchini Saudi Arabia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano   wa Kimataifa, vifo vya mahujaji wa Tanzania hadi sasa vimefikia watu nane katika tukio hilo.
Aidha, wizara hiyo ilisema imepokea jina la Hawa Amrani Khamis aliyekuwa amepotea tangu siku ya ajali hiyo kuwa amepatikana akiwa mzima.
Ilisema hadi sasa kuna mahujaji wanne wa Tanzania ambao wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali mbalimbali za Saudi Arabia na hali zao zinaendelea vizuri. 
Mahujaji hao ni  Hidaya Mchomvu, Mahjabin Taslim Khan na Ahmed Abdalla Jusab. Pia kuna mgonjwa mmoja aliyeugua tangu alipowasili nchini humo kwa ajili ya hijja anayeitwa Mustafa Ali Mchira bado amelazwa katika Hospitali ya Ansari Madina   katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Wizara hiyo ilisema hadi kufikia Oktoba 3, mwaka huu, Ubalozi wa Tanzania nchini saudi Arabia kwa kushirikiana na Tanzania Hajj Mission na vikundi vilivyopoteza mahujaji umefanikiwa kupata majina ya Watanzania 32 ambao bado hawajapatikana na kwamba jitihada za  kuwatambua zinaendelea.   
MUFTI WA TANZANIA ASIMULIA
Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abu Bakari Zuberi  Ali, amerejea nchini na kusimulia kilichosababisha maafa ya mahujaji  yaliyotokea katika mji wa Makka, Saudia Arabia.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) jijini Dar es Salaam, Mufti alisema maafa hayo yalitokea wakati mahujaji wakitoka Muzdalifa kuelekea Mina kwenye kikuta kinachoiitwa Jamaratul Aqaba kukipiga mawe.
“ Mahujaji baada ya kuondoka Muzadalifa huelekea Mina na waakifika hapo huelekea kwenye kuta cha Jamaratul Aqaba kukipiga mawe kama ishara inayoashiria kujikumbusha  kitendo alichokifanya Nabii Ibrahim,” alisema Mufti Zuberi.
Aidha, alisema wakati mahujaji hao wakielekea eneo hilio wengine walikuwa wamekwishafanya kitendo hicho ndipo kulitokea msongamano mkubwa baada ya njia ambazo kwa kawaida huwa mbili ya kwenda na kurudi kubakia moja badala ya mbili.
Mufti Zuberi alisema msongamano huo ulisababisha maafa kutokea yaliyopelekea mahajaji wengi kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa.
Aliongeza kuwa, baada ya tukio hilo alifanya utaratibu wa kuwasiliana na viongozi wa taasisi zilizokuwa na mahujaji pamoja na viongozi wa Tanzania Hajj Commission ili kujua  kama wapo mahujaji wa Tanzania wamefikwa na mkasa huo.
Alisema katika jitihada za kuwatafuta alipata fursa ya kukutana na baadhi ya mahaujaji walionusurika kwenye ajali hiyo ambao walieleza kuwa wenzao walishindwa kutoka eneo la tukio wakiwa hai.
Hali kadhalika alisema Tanzania Hajj Commission itaandaa ripoti nzima itakayoeleza mambo yaliyochangia maafa hayo na mapendekezo kisha yatawasilishwa mbele ya serikali  ya nchi hiyo.
Alisema Mahujaji waliokwenda Hiji walikuwa 3,00, huku akitilia mkazo kuwa  siku zijazo Bakwata itaweka utaratibu wa mahujaji wote kupitia baraza hilo kwa ajili ya kutambua idadi kamili.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!