Monday 26 October 2015

ELIMU DUNI INACHANGIA UKATILI WA KIJINSIA

Wanakamati katika Halmashauri ya Busokelo wakifanya igizo la ukatili wa kijinsia kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo wakati wa semina iliyoendeshwa na shirika la WiLDAF.

UKATILI wa kijinsia si jambo geni katika maeneo mengi nchini na wananchi wengi ni waathirika wa vitendo hivyo. Wadau wa masuala ya jamii zikiwemo asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali wanatekeleza mikakati mbalimbali kukabiliana na tatizo hilo, ikiwa ni pamoja na kuelimisha kupitia midahalo, warsha, semina, makonfamano, na mikutano ya wananchi kuwaeleza madhara ya ukatili huo.


Kwa mujibu wa tafsiri ya Umoja wa Mataifa (UN), ukatili ni kitendo chochote cha ukatili kikiwemo kwa misingi ya jinsia anachofanyiwa mtu yeyote kwa lengo la kumdhuru au kumuumiza kisaikolojia, kimwili, kiafya, kingono au kiuchumi. Mtu yeyote bila kujali jinsi yake anaweza kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia. Matokeo ya tafiti zilizofanywa na mashirika yanaonesha kuwa idadi kubwa ya waathirika wa vitendo hivyo ni wanawake na watoto.
Vyanzo vya unyanyasaji wa kijinsia ni vingi kulingana na aina ya ukatili, hata hivyo mila na desturi, sera na sheria kandamizi, jamii kufumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia, ni miongoni mwa sababu zinazoongeza kasi ya tatizo hilo katika jamii. Nchini Tanzania, vitendo vya ukatili wa kijinsia ambao ni wa kingono na kimwili umefikia asilimia 44. Mkoa wa Mara umekuwa ukiongoza zaidi kwa asilimia 72 ukifuatia Dodoma kwa asilimia 71, na ulio chini zaidi ni Tanga kwa asilimia 16.
Licha ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kutendeka katika jamii, suala hilo limekuwa likifumbiwa macho. Jamii imekuwa ikihusika katika kuwaficha wanaofanya ukatili huo na mashauri kuhusu vitendo hivyo yamekuwa yakimalizwa bila kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Tangu kuanzishwa kwa halmashauri ya Busokelo Oktoba mwaka 2012, imekuwa mstari wa mbele katika kupinga ukatili wa kijinsia kwa kuhakikisha matatizo hayo yanakwisha kabisa katika jamii.
Halmashauri hiyo wilayani Rungwe katika Mkoani wa Mbeya, imeweka kipaumbele kumaliza tatizo hilo hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio yanayotokana na ukatili wa kijinsia kutoka asilimia 100 mpaka kufikia 75. Wakuu wa idara ya maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii kupitia kamati iliyoundwa katika halmashauri hiyo wameweka mikakati kuhakikisha suala hilo linatokomezwa kabisa.
Baadhi ya mikakati ni kuhakikisha zinaundwa kamati za kata zitakazoweza kupambana na ukatili wa kijinsia, jamii inapata elimu ya kijinsia kupitia matukio yanayoandaliwa zikiwemo ngoma, vikundi, klabu shuleni na kuwatumia viongozi wa serikali za mitaa, watendaji wa kata na vijiji kwa kuwa ni watu wanaoishi karibu na jamii. Katika kutambua haki na usawa kwa waathirika, kamati hiyo inayoundwa na watu wa idara mbalimbali zikiwemo za maofisa ustawi wa jamii, afya, elimu, mahakama, polisi, dini, wanasheria, na wanajamii, kwa nafasi zao wamekuwa wakipinga ukatili wa kijinsia katika mazingira yao ya kazi na wanapoishi.
Kamati inayoshirikiana na shirika la Igogwe kwa kudhaminiwa na Taasisi iitwayo Walter Reed Program of Tanzania, kwa pamoja wanaielimisha jamii kuhusu madhara yanayotokana na ukatili wa kijinsia. Hata hivyo, pamoja na kupungua matukio ya ukatili wa kijinsia kwa asilimia hiyo katika halmashauri hii, imebainika kuwa suala la mimba kwa wanafunzi wa shule za sekondari limekuwa tatizo kubwa na jamii imekuwa kikwazo katika kupata taarifa hizo.
Katika utekelezaji wa mikakati ya kupambana na ukatili huo Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) la Dar es Salaam limebaini kwamba, wadau wengi pamoja na jamii kwa ujumla hawana uelewa wa kina namna ya kuwahudumia waathirika wa ukatili wa kijinsia. Shirika hilo lina mtandao unaojihusisha na haki za wanawake barani Afrika katika kukuza na kuendeleza mikakati inayounganisha sheria na maendeleo ili kuongeza ushiriki na ushawishi kwa wanawake katika ngazi za jamii, kitaifa na kimataifa.
Mojawapo ya mikakati yao inayotumika kufikia malengo ya shirika WiLDAF ni kuwajengea uwezo wanachama katika mtandao wake kupitia programu za mafunzo kwa kutumia mbinu shirikishi ikiwa pamoja na kutoa elimu. Shirika hilo limetoa mafunzo kwa wiki mbili ya nadharia na vitendo kwa wanachama wake katika kamati ya kupinga ukatili wa kijinsia kuhusu namna ya kuimarisha huduma za waathirika wa uovu huo katika halmashauri hiyo ya Busokelo.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo katika shirika hilo ambaye pia ni Ofisa Ustawi wa Jamii katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, Fransisca Makoye anawataka wanakamati kuyatumia ipasavyo mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo katika utendaji wa kazi. Mwanasheria wa WiLDAF katika kitengo cha uhamasishaji, Jacline Waya, ameipongeza halmashauri hiyo katika utendaji wake kwa kuunda kamati inayopambana na ukatili wa kijinsia.
Wayana anasema, wamekuwa wakipata shida maeneo mengi wanayokwenda kutoa elimu hiyo kwa kuwa wengi hawana nguvu kama hiyo hivyo kuwepo kwa umoja huo ni ishara tosha ya kupunguza tatizo hilo. Ofisa Ustawi wa Jamii katika halmashauri ya Busokelo ambaye pia ni Katibu wa kamati ya kupinga ukatili wa kijinsia, Agness Elikunda, anasema licha ya wanachama kupata weledi mkubwa katika mafunzo hayo, mikakati ya kupambana na ukatili huo itakwama endapo jamii haitakemea vitendo hivyo na kushindwa kutoa ushirikiano.
“Ili tuweze kuwa na taifa bora linalozingatia haki na usawa kwa binadamu wote, jamii haina budi kukemea janga hili la ukatili wa kijinsia katika maeneo yanayowazunguka,”anasema Elikunda. Jamii inashauriwa kutoa taarifa mapema sehemu husika kuhusu matukio ya ukatili wa kijinsia baada ya kuona au kugundua vitendo hivyo.
Wananchi wanapaswa kutokuwa chanzo cha unyanyapaa au kuwabagua na kuwasema vibaya waathirika wa ukatili wa kijinsia, na kushirikiana na watuhumiwa ili kupotosha ukweli na kuathiri mchakato wa kupata haki kwa kuharibu ushahidi.
Vita dhidi ya ukatili wa kijinsia inahitaji nguvu ya wote, kila mwananchi ana jukumu kubwa katika kupambana na uovu huo hasa ikizingatiwa kuwa jamii haiwezi kupata maendeleo endapo kuna watu wanatendewa maovu.
Mikakati ya kupambana na ukatili wa kijinsia si ya kibaguzi, haiwahusu wanawake au wanaume tu, ushiriki wa jamii nzima katika mapambano hayo ni silaha muhimu katika kuhakikisha kwamba utu wa kila mtu unaheshimiwa ili dunia iwe sehemu nzuri ya kuishi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!