Wednesday, 21 October 2015

Dk. Magufuli: Nitafunga kwa makufuli mianya ya ufisadi.



Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli (pichani), amewataka wananchi wa Sengerema mkoani Mwanza, kumpa kura za ushindi kwa kuwa atafunga makufuli mianya yote ya ufisadi.



 
Kadhalika, amewataka wakazi wa Sengerema na Watanzania wote, wasipoteze bahati waliyoipata kwa kumpa kura katika uchaguzi mkuu Jumapili ijayo kwa sababu ataunda Tanzania mpya ya mabadiliko.
 
Aliyasema hayo wakati wa mkutano wake wa kampeni uliofanyika mjini Sengerema mkoani Mwanza jana. “Nafahamu mianya yote inayowafanya mafisadi wavimbe kwa kiburi cha ufisadi wao, nitafunga makufuli kila kona,” alisisitiza. 
 
Aliongeza: “Mafisadi waliambiwa wajivue gamba tangu wakiwa CCM, wakakataa, lakini walipoona jina langu limepita kugombea nafasi hii, wakayavua na kukimbia,” alisema.
 
Dk. Magufuli alisema wakimchagua kuwa rais kwa miaka mitano ijayo, atafufua kilimo cha pamba na kukipandisha thamani katika soko la nje. Alisema kilimo hicho ni muhimu kwa watu wa Sengerema na kwamba kitainua uchumi na vijana watapata nafasi ya kupunguza makali ya maisha. Mgombea huyo alisema wakulima walikata tamaa ya kulima zao kubwa la biashara kwa Kanda ya Ziwa, lakini wakimchagua hawatajuta atahakikisha anawainua katika kilimo hicho. 
 
Aidha, alisema atafufua kiwanda cha kusindika na nyama na kile cha kutengeneza ngozi ili Watanzania wapate soko la nje na kukuza uchumi wa taifa.
 
“Hakuna sababu ya kusifiwa kuwa Tanzania ni nchi ya pili Afrika kwa kuwa na nyama wakati hakuna viwanda vya kusindika nyama,” alisema.
 
Kuhusu ushuru, alisema akifanikiwa kuchaguliwa, ushuru na kodi zisizokuwa na maana kwa wafanyabiashara wadogo, serikali yake itazifuta.
 
“Mwelekeo wa kubadilisha Tanzania uko katika moyo wangu na akili yangu…tumechoka ushuru wa ovyo kwa watu wa chini,” alisema. Pia aliahidi kumaliza tatizo la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yaliyotikisa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa kuwa nao wana haki ya kuishi kwani  ni binadamu kama wengine. Dk. Magufuli pia aliwanadi na kuwaombea kura wagombea udiwani na ubunge wa Jimbo la Sengerema, William Ngeleja na Charles Tizeba, wa Jimbo la Buchosa.
 
Imeandikwa na Renatus Masuguliko, Sengerema na Hellen Mwango, Dar
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!