Friday, 16 October 2015

CHOPA INAYOSADIKIWA KUBEBA MAKADA WA CCM YAANGUKA





Dar es Salaam. Chopa inayosadikiwa kubeba makada wa CCM imezua utata baada ya kudaiwa kudondoka katika eneo la Msolwa, Hifadhi ya Selous.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alilithibitishia Mwananchi kuwa kuna chopa imedondoka katika hifadhi hiyo Kitalu R3 na watu waliompa taarifa hizo walikuwa Kitalu R2.


Akizungumza na Mwananchi saa sita usiku, Nyalandu alisema eneo hilo lipo karibu na Mto Ruaha ambao ni mpana sana. “Mashuhuda waliona helkopta ikianguka na tunafanya kila kitu kuhakikisha tunapata ufumbuzi wa suala hili,” alisema Nyalandu.
Katika ukurasa wa twitter, Nyalandu aliandika, “Mashuhuda wa ajali ya helikopta iliyotokea Selous walikuwa Kitalu R2 walishuhudia ikianguka na kulipuka ng’ambo ya Mto Ruaha Kitalu R3,”
Hata hivyo, kulikuwa na utata wa hali ya abiria wanne na rubani waliokuwa ndani ya chopa hiyo iliyokuwa inatoka Dar es Salaam kwenda Iringa na Njombe.
Taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii jana usiku zilieleza kuwa helkopta hiyo ilikuwa na watu wanne na rubani mmoja.
Kutokana na taarifa hizo kuzagaa, msemaji wa Kampeni za CCM, January Makamba aliandika katika akaunti yake ya twitter kuwa: “Tumesikia habari za Chopa kuanguka huko Selous. Mungu aepushe kusiwe na majeruhi. Chopa zote zinazotumiwa na CCM kwenye kampeni ziko salama.”
Inadaiwa kuwa awali Chopa hiyo ilikuwa inatumiwa na mgombea ubunge wa Jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe.
Mwananchi ilifanya juhudi za kumtafuta Filikunjombe jana usiku, lakini simu yake muda wote ilikuwa inatumika na wakati mwingine kutopatikana kabisa.
Meneja Uhusiano wa Tanapa, Pascal Shelutete alisema wamepata taarifa za ajali lakini hakuna aliyefika eneo la tukio mpaka leo.
Aidha Meya wa Ilala, Jerry Silaa asubuhi hii aliandika kwenye kurasa yake ya Instagram kuwa: “Baba yangu Capt.William Silaa akiwa na Mhe.Deo Filikunjombe na abiria wengine walipata matatizo ya engine ya helicopter 5Y-DKK jana jioni wakitokea Dar kuelekea Ludewa. Taarifa za mwisho ilionekana imeanguka kwenye msitu wa Selous. Hakuna mawasiliano ya simu. Usiku kucha vyombo vyote vya serikali vimeendelea na jitihada za kufika eneo la tukio na jitihada kubwa zaidi zinaendelea asubuhi hii. Nawaomba wote kuwa watulivu kwani jambo hili linahitaji umakini wa hali ya juu na ushirikiano wa taasisi nyingi za wizara tofauti. Tuwaombee wote Mungu awanusuru."


No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!