Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuanzia sasa itaanza kubandika matokeo ya kura za urais kwenye vituo vya kupigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ili kuongeza uwazi na kupunguza malalamiko ya wizi wa kura.
Mpango huo umeelezwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji mstaafu Damian Lubuva alipozungumza na viongozi wa dini jijini hapa ambao walimueleza hoja hiyo kuwa moja ya vigezo vitakavyokamilisha mchakato huo kwa amani na utulivu na kuwaridhisha wagombea na wafuasi wa vyama.
Alisema licha ya kubandikwa vituoni, utangazaji wa matokeo utafanyika kama kawaida katika kila ngazi, udiwani kwenye kata, ubunge wilayani na urais Tume makao makuu.
Jaji Lubuva aliwahi kulieleza gazeti hili siku za nyuma kuwa “hakuna haja ya kuwa na shaka wala kuandaa vijana wa kulinda vituo. Hakutakuwa na nafasi hiyo kwa sababu kura zote zitahesabiwa na kubandikwa huko.
“Kila mtu atajua diwani gani kapata kura ngapi, na mbunge na hata rais aliyemchagua. Itakuwa tofauti na zamani ambapo zilikuwa zinasafirishwa na kuhesabiwa wilayani ambako watu wengine walidhani yanabadilishwa,” alisema.
Kampeni za kashfa
Aidha, viongozi wa dini wamewataka wagombea, wafuasi na wanaowanadi kuacha lugha za matusi, vitisho, kejeli na kukashifiana ili kuepuka kuchochea fujo na uvunjifu wa amani badala yake wajikite katika kunadi sera za vyama vyao.
Tamko la viongozi hao lililotolewa juzi baada ya mkutano wa viongozi hao uliofanyika jijini hapa na kuweka mikakati ya muda mrefu ya amani kwa kuishirikisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Taasisi ya Kudhibiti Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi.
“Sisi viongozi wa dini tumejiwekea makubaliano katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa amani na hatutatumia nyumba za ibada kuwa sehemu ya majukwaa ya wanasiasa,” ilisomeka sehemu ya tamko hilo lenye kurasa tatu.
Katika tamko hilo, viongozi hao wamewataka wagombea kutotumia nyumba za ibada kuonyesha ushabiki kwa chama cha siasa au mgombea yeyote katika kipindi cha uchaguzi mkuu na kuishauri NEC kutopanga upigaji kura siku za ibada.
Ushauri huo umetolewa siku mbili baada ya mgombea urais wa TLP, Mackmillan Lyimo kushauri uchaguzi huo ufanyike Jumatatu Oktoba 26 badala ya Oktoba 25 ili kutoa uhuru kwa baadhi ya watu kuabudu.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu, Damian Lubuva aliyeshiriki mazungumzo hayo, alisema Tume imeridhia kubadili siku hiyo katika siku za usoni, lakini mwaka huu ilishindikana kutokana na taratibu nyingine kukamilika.
“Huko mbele ya safari uchaguzi hautafanyika Ijumaa, Jumamosi wala Jumapili. Tumezungumza na kukubaliana hilo na maaskofu na tutalizingatia. Awamu hii ilishindikana kwa sababu Zanzibar walikuwa wameshatangaza tarehe ya uchaguzi. Maandalizi yalikuwa yamekamilika,” alisema Jaji Lubuva.
Viongozi hao wa dini pia waliitaka NEC kuweka utaratibu maalumu wa kuwaruhusu wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na watu wote watakaojiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi ujao, jambo ambalo tume hiyo ilishasema “kila aliyejiandikisha atapiga kura”.
No comments:
Post a Comment