WATOTO watatu wa familia moja katika Kitongoji cha Machawa, Kijiji cha Malonga Kata ya Milale wilayani Rorya, mkoani Mara,wameteketea kwa moto baada ya kuungulia ndani ya nyumba.
Tukio hilo lilitokea juzi mapema alfajiri mara baada ya mama mzazi wa watoto wawili kati ya watatu waliopoteza maisha,kuwaacha ndani wakiwa wamelala na kwenda katika maeneo ya mto ulio jirani na nyumbani kwaajili ya kununua mboga.
Watoto waliofariki dunia kutokanana tukio hilo ni Baraka Godfrey na Happy Iddi wenye umri wa miaka 3 kila mmoja na Bella Godfrey mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.
Shuhuda wa tukio hilo,Elisha Mugha,aliuambia mtandao huu,alishuhudia moshi ukitoka kwenye nyumba hiyo ndipo alipotoa taarifa kwa majirani wengine waliokuwa jirani na nyumba hiyo na kuamua kwenda kutoa msaada wa kuuzima moto huo.
Amesema walipofika eneo la tukio walianza kuuzima moto huo na mara ulipo pungua walishuhudia kuwepo kwa watoto watatu wakiwa tayari wameshapoteza maisha kwa kuungua na moto huo.
“Hatukujua kama kulikuwa na watoto ndani,tuliwaona baada ya moto kupungua na kuwatoa ndani wakiwa tayari wameshapoteza maisha baada ya kuungua vibaya kutokana na kukosa msaada wa haraka.
“Baada ya kuwatoa tuliwahifadhi kwenye jiko la kupikia lililokuwa jirani na wakati wote ambao tulikuwa kwenye nyumba hiyo mama wa watoto hao alikuwa bado hajarudi,”amesema shuhuda huyo
Kamanda wa jeshi la polisi kanda maalumu ya Tarime/Rorya,Lazaro Mambosasa,alisema taarifa kamili ya chanzo cha moto uliosababisha vifo vya watoto hao bado hakija julikana huku upelelezi wa kubaini chanzo chake ukiwa bado unaendelea.
Kufuatia tukio hilo,kamanda huyo ametoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano wa kubaini chanzo cha moto huo na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya majanga ya moto ambayo yamekuwa yakisababisha vifo.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilayani Rorya,Samweri Kiboye,ametoa misaada ya kibinadamu kwa familia hiyo ikiwemo vyakula,godoro,nguo,shuka,branketi,sabuni,chumvi,mchele pamoja na kiasi cha shilingi laki moja ili kuwasaidia katika kipindi hiki kigumu kwa familia hiyo.
No comments:
Post a Comment