Naibu katibu mtendaji kutoka Ofisi ya Rais Tume ya Mipango anayesimamia klasta ya Miundombinu na huduma, mhandisi Happiness Mgalula akitoa hotuba katika mkutano uliowahusisha ujumbe wa wadau wa maendeleo ya viwanda kutoka Tanzania na ujumbe wa wawekezaji kutoka nchini China.
Wajumbe wa mkutano wakiwa wanafuatilia kwa makini mada zinazowasilishwa katika mkutano wa wadau wa maendeleo ya viwanda.
Naibu katibu mtendaji kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango anayesimamia klasta ya bishara za kimataifa na mahusiano ya uchumi, Bw. Paul Sanagawe akihutubia wajumbe wa kikao ambao ni wadau wa maendeleo ya viwanda kutoka China na Tanzania.
Wajumbe wa mkutano wakifuatilia mada inayotolewa na Mkurungenzi wa viwanda kutoka wizara ya viwanda na biashara mhandisi Elli Pallangyo.
Mkurungenzi wa viwanda kutoka wizara ya viwanda na biashara mhandisi Elli Pallangyo akitoa mada kwa wajumbe wa mkutano.
Mkurugenzi mtendaji wa sekta binafsi nchini Bw. Godfrey Simbeye akisisitiza jambo wakati akiwasilisha mada kwenye mkutano ambapo aliisifu serikali kwa kujitahidi kuweka mazingira mazuri ya biashara kwa sekta binafsi.
Picha ya pamoja kati ya wadau wa maendeleo ya viwanda kutoka Tanzania na ujumbe wa wawekezaji kutoka nchini China.
Wajumbe wa mkutano wakisikiliza kwa makini hotuba kutoka kwa Naibu katibu mtendaji Ofisi ya Rais Tume ya Mipango, Mhandisi Happiness Mgalula wakati wa mkutano.
Wajumbe wa mkutano wakiwa wanasoma kwa makini baadhi ya nyaraka katika mkutano huo.
Mkurugenzi mtendaji wa kituo cha uwekezaji Tanzania (CTI) Bibi Juliet Kairuki (kulia) akibadilishana mawazo na kaimu mkurugenzi wa NDC bw. Mlingi Mkucha nje ya ukumbi wa mkutano.
Wajumbe wa mkutano wakiwa wanasikiliza kinachoendelea ndani ya mkutano wa wadau wa maendeleo ya viwanda.
Na Adili Mhina.
Wadau wa maendeleo ya viwanda nchini wametumia vyema fursa ya kutangaza na kuwashawishi wawekezaji wa kigeni kutoka nchini China kuwekeza katika maeneo muhimu yatakayohimiza maendeleo ya viwanda na kupunguza umaskini miongoni mwa wananchi.
Hayo yametokea katika mkutano wa siku mbili mfululizo kati ya wadu wa maendeleo ya viwanda kutoka serikalini, sekta binafsi nchini pamoja na ujumbe wa wawekezaji kutoka nchini China uliomalizika jana. Mkutano huo ulioandaliwa na kituo cha kimataifa cha kupunguza umaskini cha nchini China, Mfuko wa maendeleo wa China-Afrika kwa kushirikiana na kituo cha uwekezaji Tanzania na Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ulibeba ujumbe usemao, “punguza umaskini kupitia maendeleo ya viwanda”.
Katika hotuba yake kwa niaba ya katibu mtendaji wa Ofisi ya Rais Tume ya mipango, naibu katibu mtendaji anayesimamia klasta ya miundo mbinu na huduma mhandisi Hapness Mgalula alisema Mkutano huo umekuja wakati muafaka ambapo Tanzania ipo katika maandalizi ya kuandaa mpango wa maendeleo wa miaka mitano (2016/17-2020/21) ambao umebeba dhima ya kuendeleza uchumi wa viwanda. “mkutano huu sio kwamba tu umekuja wakati muafaka lakini pia ni muhimu kwa sababu miongoni mwa yatakayojadiliwa hapa yatatumika katika kuboresha huo mpango”, alisema Mgalula.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC), bi Juliet Kairuki aliueleza ujumbe kutoka China kuwa kuwa Tanzania kuna maeneo mbali mbali ya uwekezaji ambayo yanaweza kuleta tija kubwa kwa Taifa pamoja na wawekezaji. Alisisitiza zaidi kwa wawekezaji hao kuwekeza katika kujenga viwanda nchini ili kuondokana na usafirishaji bidhaa ghafi kwenda nchi za nje. Miongoni mwa maeneo aliyoyawekea msisitizo katika uwekezaji wa ujenzi wa viwanda ni pamoja na; ubanguaji wa korosho, usindikaji wa mbegu za mafuta, utengenezaji wa nguo, ngozi, utengenezaji wa nyama bora na maziwa.
Alisisitiza kuwa pamoja na kuwa uwekezaji wa ujenzi wa viwanda katika maeneo hayo utasaidia kukuza ajira kwa wanachi vilevile utasaidia kuongeza thamani ya bidhaa zinazotoka nchini kwenda kuuzwa nchi za nje. “kwa sasa bidhaa nyingi zinauzwa zikiwa ghafi na hii inafanya kuuza bidhaa bei ya chini wakati kama tukifanikiwa kujenga viwanda na kuuza bidhaa za viwandani thamani ya mazao yetu itaongezeka na italeta faida upande wa serikali na vilevile kwa muwekezaji,”.
Nae mkurugenzi wa viwanda kutoka wizara ya viwanda na biashara mhandisi Elli Palangyo aliwahakikishia wawekezaji kuwa Tanzania ni sehemu salama kwa uwekezaji hivyo yeyote anayekuja kuwekeza ajue kuwa yupo katika eneo salama na lenye tija kibiashara. Alieleza kuwa Tanzania ina faida nyingi za kuwavutia wawekezaji ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa amani na utulivu wa taifa toka kipindi cha uhuru, uwepo wa maliasili za kutosha kama vile madini na gesi asilia, upatikanaji wa ardhi ya kutosha na yenye rutuba kwa ajili ya kilimo, kuwepo kwa bahari inayotumika kupitisha bidhaa mbalimbali hususani kwenye nchi zisizo na bahari, na zingine nyingi.
Kwa upande wa Zanziabar Mkurugenzi wa uwekezaji kutoka mamlaka ya uwekezaji vitega uchumi Zanzibar (ZIP) Nasriya Nassor alieleza wadau kuwa Zanzibar ina fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta za utalii, uvuvi, kilimo pamoja na maeneo mengine kama huduma za kifedha, usafirishaji, nishati pamoja na huduma mbalimbali za jamii.
Wawekezaji hao kutoka nchini China walionesha kuridhishwa na uwepo wa fursa mbalimbali zilizopo nchini na kueleza kuwa katika kutimiza azma ya kupunguza umaskini kupitia maendeleo ya viwanda Tanzania, China ina jukumu kubwa hususani katika kutoa mawazo, uzoefu, elimu, fursa na kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment