Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mathias Chikawe, amesema, Tanzania inakabiliwa na tatizo la usafirishaji wa vijana na watoto kwa madhumuni ya ugaidi jambo ambalo ni tishio kwa jamii kimataifa.
Chikawe alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mpango kazi wa kitaifa na kanuni za sheria ya kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu.
Alisema ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, Tanzania inazalisha watu wanaokwenda kutumikishwa nje ya nchi na njia ya kuwapitisha.
“Matukio yaliyokithiri sana nchini ni usafirishwaji haramu wa watu kutoka nchi za pembe ya Afrika kuelekea Afrika Kusini, wengi hukamatwa wakiwa wametelekezwa au wakisafirishwa katika njia za hatari zisizo na ubinadamu hata kidogo,” alisema.
Alisema ripoti ya Serikali ya Marekani ya mwaka 2013 iliiweka Tanzania katika kundi la pili la viwango vyao vya uwepo wa biashara hiyo, ilionyesha kuwa matukio ya ndani ni mengi yanayohusisha vijana ambao husafirishwa na ndugu au jamaa kwa ahadi za kusomeshwa au kutafutiwa kazi nzuri mijini.
Hata hivyo, alisema waathirika wamejikuta wakifanyishwa kazi bila ridhaa na wengine kuingia katika rekodi za matukio ya unyanyasaji wa kingono hasa wasichana.
Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Ghalib Bilal, alisema kuwa, tafiti zinaonyesha zaidi ya watu 700,000 husafirishwa kutoka nchi moja kwenda nyingine kufanyishwa biashara za unyonyaji.
Aidha, alisema serikali inadhamira ya dhati ya kutokomeza tatizo hilo.
Kadhalika aliwaomba wawakilishi wa mabalozi waliofika kwenye hafla hiyo kukabidhiwa mpango huo ili nao wasaidie kwa upande wao.
No comments:
Post a Comment