Saturday, 29 August 2015

SHIRIKA LA AFYA DUNIANI LACHANGIA SH MIL 202 KUPAMBANA NA KIPINDUPINDU


Shirika la Afya Duniani (WHO) limepanga kutoa msaada wa kifedha, dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 202 kwa lengo la kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu unaoendelea kusambaa katika mikoa nchini. 

Mwakilishi Mkaazi wa Shirika hilo nchini, Dk.Rufaro Chatora, akizungumza jana mara baada ya kuikabidhi Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii msaada wa vifaa vyenye thamani ya Sh. Milioni 42.5, alisema lengo lao ni kusaidia mapambano hayo.
“Leo tunatoa msaada wenye thamani ya Sh. milioni 42.5 na tunatarajia kusaidia zaidi kwa kutoka Sh. Milioni 159.8 muda wowote kuanzia sasa, kati ya msaada huo wote fedha taslimu zitakuwa ni Sh. milioni 60” alisema.
Dk. Chatora, alisema zaidi ya Sh. milioni 159 zitatumika kwenye utoaji wa msaada wa usimamizi, huduma za kimaabara, ufuatiliaji na uhamasishaji wa kijamii.
Akichanganua msaada waliotoa jana Chatora alisema wameikabidhi serikali katoni 1,000 za dawa aina ya water guard pamoja na lita 100 za dawa ambazo kazi zake ni kutakasa na kuondoa vimelea vya magonjwa.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Donad Mmbando, aliwataka wataalamu kusimamia rasilimali hiyo vizuri kwa kuhakikisha zinawafikia walengwa.
Kuhusu ugonjwa huo, alisema licha ya juhudi za serikali kila mara kutoa tahadhari lakini bado kila mwaka Tanzania imekuwa ikikabiliwa na ugonjwa huo.
Alisisitiza kuwa, agizo la kukagua maeneo ya chakula ikiwa ni pamoja na migahawa na hoteli iendelee na wale watakaokutwa kwenye mazingira machafu, bila kujali ukubwa, zifungiwe.
Alisema kuwa kutokana na ukubwa wa tatizo serikali imekusudia kuongeza kambi za wagonjwa kutoka tatu hadi nne kulingana na uhitaji wa eneo.
Alisema kuwa fedha watakazopokea kutoka WHO zitasaidia kuimarisha vituo, vifaa na kuwaongezea motisha wataalam ambao sasa wanafanya kazi saa 24 vituoni humo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!