Saturday, 29 August 2015

RAIS KIKWETE ATOA RAMBI RAMBI TUKIO LA AJALI YA MOTO



Rais Dk. Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik, kufuatia tukio la ajali ya moto lililosababisha vifo vya watu tisa wa familia moja ya Masoud Matal, juzi alfajiri.



 
Wanafamilia hao wakiwemo watoto watano walipoteza maisha baada ya nyumba yao kuteketea wa moto katika Mtaa wa Gulam, eneo la Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam.
 
Baba wa familia, Matal alisalimika katika ajali hiyo kwa kuwa hakuwamo katika nyumba wakati ikiungua.
 
“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na nimesikitishwa mno kutokana na taarifa za kupoteza maisha kwa watu tisa wa familia moja ya Bwana Masoud Matal baada ya nyumba yao kuunguzwa na kuteketezwa kabisa na moto alfajiri ya tarehe 27 Agosti, 2015,” alisema katika taarifa yake Rais Kikwete.
 
Aliongezea “Kwa hakika hili ni pigo kubwa kwa bwana Masoud Matal, lakini namuomba awe mvumilivu kwa machungu yote ya kupotelewa ghafla na familia nzima, lakini  yote amwachie Mwenyezi Mungu muweza wa yote.” 
 
 Rais Kikwete alimuomba Sadik kumfikishia salamu zake za rambirambi na pole nyingi kwa Matal kutokana na msiba huo mkubwa, na amemuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza mahala pema peponi roho za marehemu wote.
 
Mseimaji wa famili hiyo, Suleiman Bashirafu, akizungumza Nipashe, alisema  familia imepata pengo kubwa ambalo haliwezi kuzibwa.
Alisema bado wapo katika wakati mgumu kwa kuwa Mattal  hajui hatima ya maisha yake.
 
Bashirafu alisema katika ajali hiyo hawakufanikiwa kuokoa chochote.
Aliiomba serikali imsaidie baba huyo kwani hana sehemu ya kujihifadhi kwa sasa na hana fedha za kupanga kutokana na tatizo hilo.
Aliishauri serikali kuhakikisha inaweka vituo mbalimbali vya magari ya zimamoto ili iwe rahisi kutoa huduma kwa wakati.
 
Alisema kuna haja ya wananchi kupatiwa taarifa jinsi ya kujiokoa ili waweze kupambana na matukio ya aina hayo ikiwemo kuwa na mlango wa dharura kwa kila nyumba zinazojengwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!