MICHEZO ya 11 ya Mataifa ya Afrika inafanyika Congo Brazzaville kuanzia Septemba 4 hadi 19, mwaka huu.
Ni michezo ya aina yake kwani watakuwa wakisherehekea pia kumbukumbu ya miaka 50 tangu ilipofanyika michezo ya kwanza mwaka 1965 Brazzaville, Congo. Jumla ya nchi 54 zinatarajia kushiriki katika michezo hiyo huku Tanzania ikiwa ni mojawapo ya nchi hizo, ambazo zitashindana katika michezo 22.
Michezo yenyewe
Baadhi ya michezo itakayoshindaniwa katika wiki hizo mbili ni riadha, badminton,mpira wa kikapu, soka la ufukweni, mpira wa wavu wa ufukweni, ngumi, baiskeli, soka, mpira wa mikono, judo, karate ya asili, karate ya kawaida na raga.
Michezo mingine itakayoshindaniwa humo ni kuogelea, tenisi, mpira wa meza, mpira wa wavu, kunyanyua vitu vizito, taekwondo na mchezo wa mieleka. Tayari timu ya soka ya wanawake ya Tanzania ya Twiga Stars imefuzu kwa ajili ya michezo hiyo ambayo imekuwa ikifanyika kila baada ya miaka minne.
Timu za Tanzania
Tanzania ambayo ni mshiriki mzuri wa michezo hiyo kila inapofanyika, mwaka huu inatarajia kupeleka michezo ya riadha, ngumu, soka la wanawake, michezo kwa walemavu na judo.Tayari Chama cha Baiskeli Tanzania (Chabata) kimeandika barua na kusema kuwa hakitashiriki michezo ya mwaka huu kwani kinafanya maandalizi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki itakayofanyika Rio nchini Brazil mwakani.
Mbali na baiskeli, timu ya wanyanyua vitu vizito pamoja na ile ya taekwondo nazo inaelezwa kuwa zimejitoa licha ya kutotoa taarifa rasmi ya maandishi kama walivyofanya wenzao wa baiskeli. Kwa sasa baadhi ya timu ziko katika maandalizi makali licha ya kusumbuliwa na ukata unaowafanya kushindwa kukaa katika kambi za kudumu au kupata mahitaji muhimu kwa timu hizo.
Mfano timu ya taifa ya ndondi, ambayo ilipeleka wachezaji wanne badala ya watatu katika mashindano ya majiji ya Afrika Mashariki, imekuwa ikikabiliwa na ukata na kuifanya kufanya mazoezi bila ya kuwa na vifaa.
Wachezaji wachache
Mwaka huu ukiondoa wachezaji wa timu ya soka ya wanawake, ambao watakuwa 25, timu zingine zote zitakuwa na jumla ya wachezaji 15 tu tena pamoja na makocha wao. Uchache huu unatokana na ukata wa fedha ndio unaoifanya timu hiyo kuwa na wachesaji hao wachache. Kwa wastani karibu kila timu ukiondoa soka, itakuwa na wachezaji watatu tu na kocha. Kutokana na ukata huo hakutakuwa na meneja wala viongozi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), ambao ndio waratibu wa michezo hiyo kwa hapa nchini wakishirikiana na Serikali.
Maandalizi ya Michezo
Wakati umebaki muda mfupi kabla ya kufanyika michezo hiyo, timu nyingi za Tanzania bado haziko katika maandalizi makali na hivyo kutiwa wasiwasi kuwa huenda zikaendelea kusindikiza kama ilivyo kawaida yao.
Timu ya Twiga Stars wenyewe wako katika Mbande wakiendelea na mazoezi kabla ya kuhamia Zanzibar, lakini wamekosa mechi za kimataifa za majaribio, ambazo zingeweza kuwaweka fiti zaidi na kuwapa uzoefu. Twiga Stars katika michezo hiyo itakuwa na kibarua kigumu cha kufuzu hatua ya mtoano baada ya kupangwa na wenyeji Congo, Nigeria na Ivory Coast katika hatua ya makundi, ambapo imepangwa Kundi A. Kundi B lina timu za Cameroon, Afrika Kusini, Ghana na Misri.
Timu ya riadha baadhi ya wanariadha wako Eldoret nchini Kenya kwa ajili ya maandalizi, lakini bado wanariadha hao wanatakiwa kupata viwango vitakavyowawezesha kushiriki michezo hiyo. Kwa upande wa ngumi pamoja na timu hiyo wiki hii kuwa Mombasa, Kenya kushiriki mashindano ya majiji ya Afrika Mashariki lakini bado mashindano hayo sio kipimo cha kuwawezesha kufanya vizuri Congo.
Viongozi wa vyama au mashirikisho ya michezo ambayo timu zao zinatarajia kushiriki katika michezo hiyo, wanatakiwa kuziweka kambini mapema ili ziweze kujiandaa vizuri kwa ajili ya michezo, ambayo pia itatumika kama kigezo cha kushiriki Michezo ya Olimpiki mwakani nchini Brazil.
Huko nyuma Tanzania imewahi kufanya vizuri katika Michezo ya Afrika kama mchezo wa ngumi wakati mabondia wake kama akina Rashid Matumla, Makoye Isangura, Haji Ally na wengineo waliwahi kutwaa medali za dhahabu kwa nyakati tofauti. Dawa ya kufanya vizuri katika michezo hiyo ni maandalizi tu, lakini kama tutababaisha tusishangae timu zetu zikarudi mikono mitupu na kuishia kuitwa watalii.
No comments:
Post a Comment