Tuesday, 18 August 2015

JE NI LUGHA IPI ITUMIKE KUFUNDISHIA ELIMU YA MSINGI?

Wanafunzi wengi wa elimu ya msingi wanajifunza
Hili ni swali ambalo kwa muda mrefu limekuwa likiibua mijadala katika duru za kisomi na ndani ya jamii kwa jumla.

Watu wamegawanyika katika makundi matatu, wapo wanaotaka Kiingereza, wapo wanaotaka Kiswahili na wengine wanataka lugha zote zitumike kufundishia.
Mfumo wa elimu wa Tanzania unatumia lugha ya Kiswahili pekee kama lugha ya kufundishia katika elimu ya msingi na Kiingereza kinafundishwa kama somo.
Baadaye Kiingereza hutumika kufundishia katika elimu ya sekondari, huku Kiswahili kikifundishwa kama somo.
Mwanzoni mwa mwaka, Rais Jakaya Kikwete alizindua Sera ya Elimu na Mafunzo ambayo imesisitiza matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa shule za umma. Sera hiyo pia inatambua lugha ya Kiingereza kama lugha ya kufundishia hasa kwa shule binafsi.
Sera hiyo inakosolewa na makundi mbalimbali ya watu kwa madai kwamba inamnyima mtoto wa Kitanzania uwezo wa kuhimili ushindani katika soko la ajira, ikizingatiwa kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki inaelekea kuwa shirikisho.
Watu wanaotaka Kiswahili kitumike kufundishia elimu ya msingi na sekondari wanatetea hoja yao kwamba Kiswahili ni lugha yenye asili ya Tanzania. Kwa hiyo, kama Taifa hili halitatumia lugha ya Kiswahili basi lugha hiyo haitakua.
Pia, kundi hilo linasema Kiswahili ni lugha ambayo inawaunganisha Watanzania; kutumika kwa lugha hii kutaongeza umoja na mshikamano wa Watanzania, sambamba na kudumisha amani.
Kundi jingine linalopendekeza Kiingereza kitumike kufundishia, linasema hiyo ndiyo lugha ya kimataifa ambayo inatumika duniani kote. Watanzania wakitumia lugha hii watanufaika na fursa mbalimbali zinazojitokeza sehemu mbalimbali duniani.
Utafiti wa Twaweza
Hivi karibuni, Taasisi ya Twaweza ilitoa matokeo ya utafiti juu ya lugha ipi hasa itumike kama lugha ya kufundishia elimu ya msingi. Utafiti huo umebaini kuwa watu sita kati ya 10 wangependa Kiingereza kiwe lugha ya kufundishia katika shule za msingi na sekondari.
Watu 1,381 wenye elimu tofauti  walihojiwa katika utafiti huo uliofanyika Tanzania Bara kwa njia ya simu za mkononi 
Mshauri wa Twaweza, Profesa Kitila Mkumbo anasema asilimia 63 ya waliohojiwa walisema wanataka watoto wao wafundishwe kwa lugha ya Kiingereza katika shule za msingi na sekondari.
Anasema wazazi wa watoto walio shule za msingi walisema kubadili lugha kutoka Kiswahili kwenda Kiingereza kutaleta matatizo. Anasema asilimia 89 ya wazazi hao walikubali kuwa kuna changamoto, huku asilimia 10 wakisema hakuna matatizo.
Walipoulizwa kuhusu ubora wa elimu ya msingi, anasema asilimia 64 ya wazazi walisema uko vizuri; asilimia 62 ya wazazi wenye elimu ya sekondari walisema iko vizuri na asilimia 50 ya wenye elimu ya juu walisema elimu ya msingi ni nzuri.
“Hapa utagundua kuwa elimu aliyonayo mzazi pia inasaidia katika kufanya uamuzi sahihi. Hiyo asilimia 64 waliyosema elimu ya msingi ni nzuri, wao pia wana elimu hiyo, kwa hiyo wengi wao pia hawana ujuzi wa upeo mkubwa,” anasema.
Profesa Mkumbo anasema matarajio ya wazazi hao pia yalikuwa tofauti. Wazazi wengi walitaka watoto wao wafanye kazi za udaktari na ualimu. Asilimia mbili tu walisema wangependa kuona watoto wao wakijikita kwenye kilimo ambacho wengi wanakitegemea.
Mkurugenzi wa ukaguzi na udhibiti wa shule nchini, Marystella Wasena anakiri kuwa kuna shida kubwa katika kuchagua lugha ya kufundishia. Anasema mtu akitumia lugha ambayo haijui vizuri atashindwa kujiamini na kufanya jambo la maana.
Anasema ni jukumu la kila Mtanzania kutafakari namna ya kulitoa Taifa katika mkanganyiko uliopo. Wasena anasema lengo kuu ni kumpatia mwanafunzi elimu ambayo itakuwa na athari chanya kwenye jamii anayotoka.
“Inawezekana mitalaa yetu iko vizuri lakini namna inavyotolewa ikawa ndiyo tatizo. Sera ya elimu ni nyumbufu, imetoa uhuru wa kutumia lugha ya Kiswahili au Kiingereza kama lugha ya kufundishia,” anabainisha mkurugenzi huyo.
Wasena anasisitiza kuwa watu wasiangalie matumizi ya lugha ya Kiswahili pekee, bali waonyeshe na upungufu mwingine kama vile mitalaa, namna elimu inavyotolewa, miundombinu ya shule au nyenzo za kufundishia.
“Miaka mitano iliyopita ufaulu wa somo la Kiswahili haukuwa mzuri licha ya kuwa Kiswahili ni lugha inayozungumzwa. Kwa hiyo, lugha isiwe hoja sana, kuna haja ya kuangalia mfumo mzima wa elimu yetu,” anasema Wasena.
Maoni ya wadau
Wadau mbalimbali wa elimu wanasema Serikali pia ina wajibu wa kufanya utafiti ili kubaini lugha inayofaa katika kufundishia watoto. Wanasema lugha ni nyenzo ya kukuza uchumi wa kuleta maendeleo ya Taifa.
Aliyekuwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Uttoh anasema hakuna namna yoyote nchi hii inaweza kukwepa kuwa nchi inayotumia lugha mbili.
Uttoh anasema siyo rahisi kutoka kwenye lugha ya Kiswahili na kwenda moja kwa moja kwenye lugha ya Kiingereza. Anaongeza kuwa lazima maandalizi yafanyike ikiwemo kuwaandaa walimu, kuandaa mitalaa na vitendea kazi.
“Sera ya elimu iko very clear (wazi), inatoa uhuru wa kutumia lugha zote mbili kwa wakati mmoja. Hata nchi nyingine pia zinafanya hivyo, kwa hiyo tusiibeze sera ya elimu, jambo la msingi ni kusimamia utoaji wa elimu hii,” anasema.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala anasema Tanzania haiwezi kuepuka lugha ya Kiingereza kama inataka maendeleo ya haraka. Anasema lugha ya kufundishia imeligharimu Taifa hili kwa kuzalisha vijana ambao hawawezi kuchamgamana na wenzao wa nchi nyingine.
 “Sera ya elimu nayo ni mbovu. Ilitakiwa iweke wazi lugha moja ya kufundishia kwa shule zote Tanzania badala ya kutoa uhuru kwa shule kuchagua zenyewe lugha ya kufundishia,” anafafanua mwanazuoni huyo.
Mwanafunzi aliyeingia kwenye kumi bora ya matokeo ya kidato cha sita mwaka huu, Kelvin Fidelis anasema lugha ya Kiingereza inafaa kufundishia shule za msingi kwa sababu itawajengea wanafunzi msingi mzuri wanapokwenda sekondari.
“Wanafunzi wengi wanapata shida wanapoingia kidato cha kwanza na kukuta lugha ya Kiingereza ambayo hawaijui. Mimi nilisoma shule inayotumia lugha ya Kiingereza, sikupata shida, lakini wapo wenzangu ambao walikuwa wanachukua muda mrefu kuelewa,” anasema.
Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Lukangao, Innes Tawata anasema huu ni wakati wa sayansi na teknolojia na dunia imekuwa kama kijiji, kwa hiyo lugha ya Kiingereza inatakiwa kufundishwa kikamilifu bila kukitupa Kiswahili.
“Siku hizi ukienda kwenye usaili  unaambiwa lazima ujue kuongea Kiingereza. Kwa mfumo huu Taifa letu linazalisha nguvu kazi ambayo haiwezi kukidhi mahitaji ya soko la ajira,” anasema mwalimu huyo.
Utafiti umefanyika, wadau wamezungumza; sasa ni wakati wa Serikali kusikiliza hoja za wananchi na kufanya utafiti wake ili iweze kufanya uamuzi sahihi katika kujibu swali ambalo pengine majibu yake ya sasa hayaridhishi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!