Bandari ya Dar es Salaam inaingia katika historia mpya nyingine leo wakati meli ndefu kuliko zote zilizowahi kufunga katika bandari hiyo itakapoingia.
Meli hiyo yenye urefu wa mita 255, inatarajiwa kutia nanga nchini na kufunga gati kesho Kampuni ya Kuhudumia Makontena nchini (Ticts) katika Bandari ya Dar es Salaam.
Meli hiyo inayojulikana kama Clemens Schulte, ina uwezo wa kubeba makontena 5,466 na inamilikiwa na moja ya kampuni kubwa duniani ya meli ya Maersk Line.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja wa Mawasiliano wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Janeth Ruzangi, alisema kuwasili kwa meli hiyo kutoka bandari ya Laem Chabang ya nchini Thailand, ni uthibitisho wa kuongezeka kwa kuaminika kwa Bandari ya Dar es Salaam.
“Bandari yetu inazidi kuaminika zaidi kadiri siku zinavyokwenda kutokana na kuimarishwa kwa huduma pamoja na ulinzi na usalama wa mali za wateja,” alisema.
Mkurugenzi wa Maendeleo Ticts, Donald Talawa, alisema mara ya mwisho kampuni hiyo kupokea meli kubwa ilikuwa Februari, 2014 ambapo meli ya Msc Martina iliyokuwa na urefu wa mita 242, ilitia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam.
Wakati wa safari hiyo ya kwanza, inatarajiwa kwamba MV Clemens Schulte, itashusha makontena 250 na kupakia mengine 1,300, alifafanua Talawa
No comments:
Post a Comment