Friday, 28 August 2015

BENKI YA DUNIA YATOA SH 422 BILIONI KUSAIDIA UBORESHWAJI HUDUMA ZA AFYA TANZANIA


Benki ya Dunia (WB), imeipatia Serikali ya Tanzania mkopo wa Dola milioni 200 za Marekani (sawa na Sh. bilioni 422) kwa ajili ya kusaidia uboreshaji wa huduma za afya kwa wajawazito na watoto wachanga.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Sebastian Likwelile, alisema serikali itahakikisha fedha hizo zinazaa matunda kwa wakati.
“Kwanza niishukuru Benki ya Dunia kwa kutupa mkopo wenye riba ndogo na ya muda mrefu kwa ajili ya kusaidia uboreshaji wa huduma za afya kwa mama na mtoto kutokana na kundi hili kukabiliwa na changamoto nyingi,” alisema Likwelile.
Aidha, alisema pamoja na kuwapo kwa mikakati mbalimbali ya kupambana na changamoto hizo, bado kuna kazi kubwa kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa ili kupunguza vifo ambavyo si vya lazima kwa wajawazito na watoto wachanga.
"Serikali imekuwa ikipambana kupunguza tatizo hili na kufanikiwa kwa kiwango kidogo kutokana na upungufu wa vifaa ambapo mwaka 2010 wajawazito 454 kati ya 100,000 walifariki dunia," alisema.
Aliongeza kuwa watoto 26 kati ya 1,000  wenye umri wa kati ya miaka mitano, hufariki dunia kutokana na magonjwa mbalimbali na wengine wakati wa kuzaliwa.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Bernad Konga, aliishukuru WB kwa mkopo huo na kusema kuwa utasaidia kwa kiwango kikubwa kuimarisha huduma za afya.
"Tunaahidi kuwa fedha hizo zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuhakikisha vifo vya watoto wachanga na wanawake wakati wa kujifungua vinapungua," alisema Konga.
“Sekta ya afya inakabiliwa na changamoto nyingi lakini kwa kutumia fedha hizi, tutahakikisha zinatatuliwa kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo,” alisema Konga.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!