Monday, 31 August 2015

ASKOFU: MSICHAGUE VIONGOZI WENYE MAKANDOKANDO MENGI


ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Dk Barnabas Mtokambali, amewataka Watanzania kumkataa mgombea mwenye makandokando ya ufisadi na rushwa na kuelekeza nguvu kwenye masanduku ya kura ili wezi na mafisadi wasipate uongozi.


Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya Idara ya Wanawake (WWK) ya Kanisa hilo yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Mjini hapa.
Alisema wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu ni muhimu wananchi wakajihadhari na watu wanaotafuta kuingia madarakani na kuangalia uwezo wa mgombea awe wa Urais, Ubunge au Udiwani kama kweli ana uwezo wa kuongoza.
Askofu Mtokambali alisema ni muhimu sana wananchi kumkataa mgombea anayejihusisha na ufisadi na rushwa na kuacha kuwachagua viongozi wa aina hiyo bila kujali anatoka chama gani.
“Ukiweka nyani hawezi kumsimamia nyani mwingine, ni lazima watamaliza mahindi shambani na nguvu zote zielekezwe siku ya kupiga kura ili viongozi wa aina hiyo wasichaguliwe,” alisema.
Aliwataka pia wanawake watumishi Wakristo na Watanzania kwa ujumla kuomba mfululizo ili maadui wa ndani na nje washindwe kwani nyakati hizi hupenda kujipenyeza na kufanya kazi zao ili apatikane kiongozi kutoka kwa Mungu ili amani na upendo viendelee kuwepo nchini.
Askofu Mtokambali alivitaka vyama vyote kufanya kampeni kwa amani na utulivu pamoja na vyombo vya habari kutenda haki na si kupika habari na kupotosha jamii.
Alitoa mfano kuwa vita vilivyotokea nchini Rwanda sababu kubwa ilikuwa ni vyombo vya habari kupotosha taarifa. Askofu huyo alitaka nyumba za ibada kutotumika kama nyumba za kampeni kwa ajili ya wagombea na pia akaitaka Tume ya Uchaguzi kutenda haki kwa kutangaza washindi kwa wakati.
Kwa upande wake mshauri Mkuu wa wanawake Wakristo, Gladmary Mtokambali alisema serikali imetoa mchango mkubwa kutokana na kuendesha huduma kwa amani na utulivu na kuwataka Watanzania kuendelea kuilinda amani ya nchi iliyopo.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa alisema wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu lazima wananchi kuwa makini ili nchi ipate kiongozi mwenye uwezo wa kuongoza nchi na kuachana na ushabiki usio na maana yoyote ile. Katika risala wanawake hao iliyosomwa na Faraja Hamuli, walisema wamekuwa wakimuomba Mungu ili atoe kiongozi atakayetoka kifuani mwake.

HABARI LEO.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!