Sunday, 16 August 2015

ASHA JUMA: ANAPAMBA KUWA DAKTARI KUTIMIZA NDOTO YA MAMA


KATIKA malezi ya familia, watoto wengi hutazama mwenendo, maisha na matamanio ya wazazi wao na kupenda siku moja kufanya jambo litakaloridhisha wazazi hao au kuja kuwa kama mzazi wake. Ndivyo ilivyo kwa msichana Asha Juma (16), anayesoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Kinzudi iliyopo Goba jijini Dar es Salaam.


Asha anasema ndoto yake anatamani kuwa daktari bingwa, ndio maana ameamua kufanya bidii katika masomo yake, ili kutimiza ndoto hiyo baadae. Akizungumzia sababu ya kuwa na ndoto hiyo, Asha hafichi kwamba ndoto hiyo zamani ilikuwa ya mama yake, ambaye alipenda kuwa daktari, lakini kwa bahati mbaya haikutimia, lakini mpaka leo anatamani kuifanya kazi hiyo.
Mbali na kuwa ni ndoto ya mama yake ambayo haikutimia na yeye anataka kuitimiza, Asha anasema hata yeye tangu akiwa shule ya msingi, alijikuta akitamani kuwa daktari bingwa kwa kuwa kila alipokwenda hospitali na kuwaona madaktari wakiwa wamevalia makoti yao, wamekuwa wakionekana nadhifu hivyo anafurahia hali hiyo. “Ninaipenda kazi ya udaktari. Pia ninapokwenda hospitali ninajisikia raha madaktari walivyo, wanavyovalia. Ninavutiwa nao,” anasema.
*Jitihada darasani
Historia ya Asha darasani inaonesha jitihada zake katika kutimiza ndoto zake, ambapo anasema tangu akiwa shule ya msingi, amekuwa akiongoza darasani na kwa kumbukumbu zake, darasa la tatu alikuwa wa tatu na darasa la nne mpaka la saba alikuwa wa pili. Baada ya kumaliza shule ya msingi, Asha anasema jitihada zake hazikukoma na ndoto yake bado iko hai ndio maana tangu kidato cha kwanza mpaka cha tatu alichopo hivi sasa, amekuwa wa kwanza.
Mwanafunzi huyo anasema baada ya jitihada zake za kujifunza, kila anapoona matokeo yake kwamba kaongoza wenzake, amekuwa akijisikia furaha kwa kuwa anaamini kwa siku za mbeleni atakuwa na maisha mazuri baada ya kutimiza ndoto ya kuwa daktari. “Na maisha mazuri hayo hayapatikani bila kusoma kwa bidii. Maisha yenyewe bila kusoma kwa bidii utahangaika,” anasema mwanafunzi huyo.
Anaeleza kuwa mara nyingi anapofanya vizuri katika masomo, wazazi wake wamekuwa wakimpa vifaa vya shule ili kumtia moyo zaidi ikiwemo madaftari, vitabu na mabegi. Vivyo hivyo kwa walimu wake shuleni wanafunzi wanaofanya vizuri hupewa vifaa mbalimbali vya shule. Anasema inapoonekana ameshuka kimasomo walimu humwita na kumsaidia pamoja na kumshauri nini cha kufanya.
“Ninaposhuka kimasomo walimu huniita na kuniambia nikazane sana katika masomo. Pia pale ninapoonekana sijafanya vizuri hunishauri niongeze bidii kusoma,” anasema. Ili kuhakikisha hashuki kwenye kiwango anataka kufikia anasema huwa binafsi anasoma sana pia hushirikiana na wenzake kusoma. Husoma na wenzake kwa majadiliano na kubadilishana nyenzo mbalimbali za kusomea. Pale mmoja wao asipoelewa jambo huuliza kwa yule anayeelewa.
Asha anajua ndoto yake ili itimie, lazima asome masomo ya sayansi ambayo ni Hisabati, Fizikia, Kemia, Bayolojia, Uraia, Kiswahili, Kiingereza na Jiografia. Anasema kwa ujumla anafaulu masomo yote ila Kiswahili ndio kinamuwia vigumu kidogo katika eneo la viambishi. Mwanafunzi huyo anaeleza kuwa anajitahidi zaidi ili asishuke kielimu kwa kujiwekea ratiba yake ya kujisomea.
Anawataja walimu wanaomfundisha kwa jina moja moja kuwa somo la Hisabati na Fizikia ni Mwalimu Lucas, Kiingereza ni Mwalimu Ntambala, Kemia ni Mwalimu Msangya, Bayolojia Mwalimu Pili, Uraia Mwalimu Shadrack Ndambo na Jiografia Mwalimu Hamenya Paul. Anapopata shida ya kimasomo, anasema kwake ni rahisi kumweleza Mwalimu Mwinyimvua.
*Nidhamu ya muda
Katika jitihada za kufanikisha malengo yake, anasema amejiwekea ratiba ya kujisomea, ambayo inazingatia muda wa mapumziko na hata muda wa ziada akiwa darasani. Kwa mfano, anasema mwalimu asipoingia darasani hutumia muda huo kujisomea.
Pia wanapotoka darasani jioni saa 10, hutumia muda wa saa moja kujisomea kabla ya kwenda nyumbani. Siku za Jumamosi awapo nyumbani, hutumia masomo matatu mpaka manne kila somo hulipa muda wa nusu saa na akiwa shuleni baada ya kutoka husoma masomo mawili kila siku.
Pamoja na kujisomea, Asha anasema amekuwa pia akisaidia kazi za nyumbani ambapo anasema kuwa kila anaporudi nyumbani, husaidia kupika na kuosha vyombo jioni na siku za mapumziko kama Jumamosi na Jumapili, hufagia, kufua na kupika.
Naye mwalimu wake wa taaluma, Da- vid Seuya anamzungumzia mwanafunzi huyo kuwa kitaaluma ni mzuri. “Anajitambua. Sisi kama wataalamu ama walimu tunaanza kumwona mtoto ana uwezo mzuri kwenye matokeo ya mtihani wa Taifa,” anasema Seuya.
Anasema mtihani wa Taifa wa Kidato cha Pili, mwanafunzi huyo alifanya vizuri na alipata alama za A kwa masomo nane. Kwa mujibu wa Mwalimu Seuya, Asha alifaulu kwa kiasi kikubwa kwa kidato cha pili na hata katika kidato cha tatu ameonekana ni mtoto anayeuliza maswali, anajitambua na kama hajui sehemu anauliza maswali.
Katika suala la nidhamu mwanafunzi huyo ni Dada Mkuu wa Shule ambapo Mwalimu Seuya alisema mpaka kupata nafasi hiyo, ni kwamba ana nidhamu nzuri, ana heshima kwa walimu na wanafunzi wenzake.


Mwalimu huyo wa taaluma anasema changamoto ambazo zinaweza kukwamisha taaluma ni vifaa vya kujifunzia. “Tumejengewa maabara lakini vifaa hakuna. Mtaala unabadilika mara kwa mara, sera ya elimu inabadilikabadilika inamfanya mwanafunzi hapati kile kinachofundishwa,” anasema.
HABARI LEO

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!