Dar es Salaam. Mgombea urais wa Chama cha ACT- Wazalendo anatarajiwa kujulikana leo pale atakapojitokeza kuchukua fomu ya kuomba kuwania nafasi hiyo katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Hatua hiyo imekuja baada ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyokutana kuzi kuazimia kusimamisha mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, huku ikisita kutaja jina badala yake ikisema atajulikana wiki hii.
Kiongozi wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe alisema mgombea huyo atakwenda leo NEC kuchukua fomu za kuwania nafsi hiyo.
Juzi, akitoa maazimio ya Kamati Kuu, Katibu Mkuu wa ACT–Wazalendo, Samson Mwigamba alisema mbali na suala la urais, kikao hicho kilijadili na kupitisha majina ya wagombea ubunge Tanzania Bara na wawakilishi wa Zanzibar.
Mwigamba alisema wagombea waliopitishwa watakiwezesha chama hicho kupata wabunge wazuri watakaobadili mwelekeo wa Bunge.
Majina ya wagombea ubunge yaliyopitishwa ni 152 kati 215 Tanzania Bara na 40 ya Zanzibar huku mengine yakitarajiwa kutangazwa baadaye kutokana na mchakato unaoendelea katika maeneo yaliyokumbwa na kasoro kwenye kura za maoni.
Miongoni mwa majina yaliyopitishwa ni ya Zitto anayegombea Kigoma Mjini na Mwenyekiti wa ACT –Wazalendo, Anna Mghwira anayewania Jimbo la Singida Mjini.
Alisema baada ya kupitisha majina ya wabunge kinachofuata wiki hii ni kutangaza jina la mgombea wa urais na jukumu hilo limeachwa katika kamati yake ya uongozi.
Kuhusu jina la mgombea urais kuchelewa kutajwa, Mwigamba alisema ACT – Wazalendo kipo makini hakikurupuki kwenye jambo hilo, hivyo wanachama na Watanzania wawe watulivu ndani ya wiki hii kila kitu kitawekwa hadharani.
“Mgombea tutakayemsimamisha ni mtu safi, hana harufu ya rushwa wala ufisadi kila Mtanzania atampenda,” alisema Mwigamba.
No comments:
Post a Comment