Mamia ya wakazi wa Wilaya ya Sengerema na Mkoa wa Geita jana walijitokeza katika mapokezi ya mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli yaliyopambwa na mbio za wapiga kasia katika Ziwa Victoria.
Dk Magufuli akitokea Mwanza, alivuka Ziwa Victoria na kuingia Sengerema huku wavuvi waliokuwa wakitumia mitumbwi wakipeperusha bendera za CCM na kukizunguka kivuko cha Mv Misungwi alichokuwa ameabiri pamoja na msafara wake.
Msafara wa Dk Magufuli ulioanzia kwenye Kivuko cha Busisi saa 3.35 asubuhi ulisimamishwa mara kadhaa na wananchi ambao walikuwa wamefunga barabara wakiwa na matawi ya miti na wengine wakitembea kuusindikiza.
Dk Magufuli ambaye alikuwa ameambatana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Rajabu Luhwavi alikuwa akisimama kwenye gari la wazi na kuwapungia wananchi waliyokuwa wamejipanga kwenye Barabara Kuu ya Geita- Bukoba.
Mapokezi ya Dk Magufuli yaliongozwa na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja ambaye gari lake ndilo lililokuwa limetangulia huku likisimama kwenye makundi ya watu na kuwapanga kutokana na wingi wao. Msafara huo pia uliongozwa na ving’ora vya polisi, huku ukiwa umetawaliwa na magari ya wabunge wa CCM kutoka mikoa mbalimbali ya Kanda ya Ziwa.
Geita yarindima
Msafara wa Dk Magufuli ulifika mkoani Geita saa 5.30 asubuhi na barabara zilifungwa kwa dakika 15 wakati mgombea huyo akisalimiana na wakazi wa mkoa huo.
Akizungumza wakati akisalimiana na wakazi wa Sengerema na Geita, Dk Magufuli alisema amepita kuwasalimu na huku akiwaahidi kuwa hatawaangusha...
“Nimekuja kuwasalimia, itoshe kusema kwamba sitawaangusha. Nimefundisha shule ya Sekondari Sengerema hivyo hapa ni nyumbani,” alisema Dk Magufuli.
Awali, Dk Magufuli alianza kwa kuimba wimbo wa Kisukuma, “aliselema” huku wananchi wakiitikia ‘alija’ “aliselema”, ‘alija’ “selema, selema, aleja, ng’wana ngosha, ‘aleja.’ Wimbo huo unamaanisha “anasukuma, anakwenda, mtoto wa kiume, anakwenda.”
Baada ya kuimba wimbo huo, Dk Magufuli alianza kwa kuwashukuru wananchi wa Geita kwa mapokezi makubwa ambayo hayajawahi kutokea tangu awe kiongozi... “Wana Geita nawashukuruni sana kwa mapokezi haya... yanaonyesha ni mapokezi ya ushindi, nimebaki na deni kubwa kwenu, nitawatumikia wananchi wote na sitawaangusha, sitajali chama nitawatumikia wote wa CUF, UDP, Chadema, CCM sitajali huyu ni wa chama gani, nashukuru sana wananchi wa Geita,” alisema na kuongeza: “Leo si siku ya kampeni, nikianza watasema nimeanza kampeni mapema. Mimi napenda kusema kwamba wanashukuru sana wana Geita kwa sala zenu zilizonifikisha hapa leo, nitafanya kazi kwa ajili ya Watanzania wote, sitawabagua.”
No comments:
Post a Comment