MUUNGANO wa Taasisi zinazoshughulikia maradhi yasiyoambukiza Zanzibar (ZNCDA) umeishauri Serikali na Mashirika wahisani kuelekeza nguvu zao katika mapambano dhidi ya maradhi hayo kwa vile hivi sasa yamekuwa tishio kwa maisha ya wananchi kuliko maradhi mengine yoyote Zanzibar.
Mratibu wa ZNCDA, Omar Abdallah Ali alitoa ushauri huo jana wakati wa upimaji wa afya za wananchi wa shehia za Karakana, Chimbuni na Mwembemakumbi, Mkoa Mjini Magharibi Unguja, kwenye Kituo cha Afya cha Karakana.
Alisema maradhi ya shinikizo la damu, kisukari na saratani yamejitokeza kuwa tishio kwa wananchi kutokana na uelewa wao mdogo juu ya maradhi hayo na wengi kutokuwa na mwamko wa kupima afya zao.
Alizitaja sababu zinazochangia kuongezeka maradhi yasiyoambukiza kuwa ni mabadiliko ya mfumo wa maisha ambao wananchi hupenda zaidi starehe kuliko kujituma, uvutaji sigara, ulevi wa kupindukia na kutumia chakula cha makopo kilichotiwa kemikali.
Akitoa takwimu ya maradhi hayo, Omar alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2011 asilimia 33 ya wananchi wa Zanzibar wanakabili na shinikizo la damu na asilimia nne wana maradhi ya kisukari na taarifa kutoka Hospitali ya Ocean Road Dar es Salaam zinasema kuwa kila mwaka wanapokea kiasi cha wagonjwa 1,000 wa magonjwa ya saratani kutoka Zanzibar.
Aliongeza kuwa saratani ya matiti na shingo ya kizazi kwa akinamama na tezi dume kwa wanaume zinaongoza kati ya wagonjwa wanaopelekwa huko kupatiwa matibabu.
Alisema taarifa hizo zinatisha kutokana na idadi ndogo ya wananchi wa Zanzibar na ni sababu iliyopelekea ZNCDA kufanya juhudi ya kutoa taaluma kwa wananchi, kuwapima afya ndani ya shehia zao na kuwapa ushauri unaofaa wa kujikinga na maradhi hayo.
Aliwataka wananchi kuanzisha utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kujua afya zao mapema badala ya kusubiri kuathiriwa na maradhi ndipo wakimbilie hospitali.
Aliwashauri viongozi wa Serikali za mitaa, wabunge, wawakilishi na madiwani, kuwasaidia wananchi kwa kuwawekea vifaa vya kupima afya zao katika sehemu wanamoishi kwa vile vifaa hivyo havina gharama kubwa.
Jumla ya wananchi 174 kutoka shehia hizo tatu walipata nafasi ya kuangaliwa afya zao na maradhi ya shinikizo la damu yamegundulika kuongoza katika shehia hizo.
No comments:
Post a Comment