WAKATI wafugaji na wafanyabiashara wa mayai ya kware wanahimiza wananchi kula mayai mengi ili kutibu magonjwa mbalimbali, wataalamu wa afya wanaonya kuwa mayai hayo yakitumiwa kwa wingi yanaongeza magonjwa.
Katika siku za hivi karibuni wafugaji na wafanyabiashara wa mayai ya kware wamekuwa wakihamasisha wananchi kula mayai hayo kwa wingi kwa madai kuwa yanaponya magonjwa mbalimbali. Baadhi ya madaktari wanasema huenda mayai ya kware anayeishi katika mazingira yake ya asili yana uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali lakini ufugaji wa sasa wa ndege hao wa mwituni unatia mashaka.
Madaktari hao wanafafanua kuwa ndege hao wanapokuwa mwituni katika mazingira ya asili wanajitafutia vyakula vinavyosaidia kutaga mayai bora na ambavyo havipatikani katika kware wanaofugwa kwenye mabanda ya ufugaji wa kisasa jambo linaloweza kusababisha watumiaji wa mayai kupata magonja zaidi badala ya kutibu. Jarida la Watafiti wa Lishe nchini Uingereza linasema yai la kware huitwa “Super- Food” yaani chakula bora kutokana na kuwa na faida nyingi katika afya ya binadamu hasa kusaidia kupambana na utapiamlo.
Jarida hilo linaeleza kuwa yai la kware ni moja kati ya vyakula vyenye virutubisho vingi muhimu na kwamba kila mtu anatakiwa ale moja kwa siku. Gazeti la Lishe na Sayansi ya Chakula la Uingereza limeandika namna watafiti hao wanasisitiza umuhimu wa nafasi ya yai la kware katika kinga nzuri ya mwili, kupunguza unene na kutunza mwili wa binadamu.
Dokta Carriel Ruxton ambaye ni Kiongozi wa utafiti huo anasema yai la kuku lina nafasi ya kiafya kwa mwili wa binadamu, utafiti huo uliainisha kwamba yai la kuku halina kalori za kutosha, bali yana protini na vitamini nyingine muhimu sana kwa binadamu kama Vitamini D na B12. Inadaiwa kuwa mayai ya kware yamethibitishwa kuwa ni chanzo kikuu cha vitamin A, B1, B2, B6, B12 na Vitamin D pamoja na kuwa na madini ya chuma, zinki, shaba na virutubisho vingine.
Pia inaelezwa kuwa mayai hayo yana amino asidi ambayo yanaliwezesha yai hilo kuwa chakula muhimu kwa lishe ya binadamu. Kwa mujibu wa wataalamu wa tiba za asili, mayai ya kware yanaweza kuimarisha kinga ya mwili na kuongeza ubora wa damu hivyo kuzuia magonjwa ya shinikizo la damu. Wanadai kuwa ili kuboresha kinga ya mwili, utumiaji wa mayai 60 unahitajika ambapo mwanzo mtumiaji anatakiwa kutumia mayai matatu na baadaye mayai matano kwa siku.
Hata hivyo, Daktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha Maabara, Matandala Luhongedzo anasema kuwa mayai ya kware hayana tofauti na mayai ya kuku ambapo mtu anapaswa kula mawili tu kwa siku na kwamba uhamasishaji wa kula mayai mengi umeegemea zaidi maslahi ya kibiashara kuliko afya ya mlaji. Anasema mayai ya kware huenda yanaweza kutibu magonjwa mbalimbali lakini endapo mgonjwa hatafuata ushauri wa daktari anaweza asipone magonjwa yanayomsumbua.
Dk Luhongedzo anasema idadi kubwa ya magonjwa ya binadamu husababishwa na tabia hivyo mgonjwa asipoacha tabia fulani hawezi kupona hata kama atakula mayai ya kware kwa wingi. ‘’Kwa mfano, magonjwa ya shinikizo la damu mara nyingi husababishwa na msongo wa mawazo ambao unatokana na tabia ya mtu, hivyo kama hata acha tabia yake ya kuwaza mambo yanayochochea shinikizo la damu, hata akila mayai 500 hawezi kupona,’’ Luhongedzo anafafanua.
Akizungumzia suala la Kinga ya mwili Luhongedzo anasema kwa kawaida binadamu huzaliwa akiwa na kinga ya mwili lakini kinga hiyo huweza kupungua kutokana na sababu mbalimbali hivyo suala la kula mayai pekee halisaidii kuongeza kinga hiyo. anasisitiza kuwa ni vyema kwa mgonjwa ambaye anataka kutumia mayai ya kware kuhakikisha anaacha tabia zote zinazochochea magonjwa ikiwa ni pamoja na kuzingatia kanuni za kula mayai mawili tu kwa siku.
Anasema kwa mgonjwa wa Virusi vya Ukimwi anatakiwa kufuata ushauri wa daktari kwani mayai ya kware pekee hayawezi kuongeza CD 4 za mwili wake. ‘’Hii ni biashara tu kwani kila mfugaji anatafuta mbinu za kupata soko kwa wingi zaidi wanawashawishi watu kwamba wakila kwa wingi mayai ya kware wanaweza kupona magonjwa mbalimbali,’’ Luhongedzo anaeleza.
Anaendelea kusema,‘’Hatumzuii mtu yeyote kula mayai hayo lakini wanatakiwa kufuata ushauri wa madaktari pamoja na kuacha tabia ambazo zinachangia magonjwa hayo.’’ Anasisitiza kuwa wagonjwa wote ambao wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali wanatakiwa kula mayai kuboresha afya zao na sio kwamba mayai pekee ndio yatawasaidia wagonjwa kupona magonjwa yanayowakabili.
Ofisa Mahusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Gaudencia Simwanza anaunga mkono maelezo ya Luhongedzo kuwa kila binadamu anatakiwa kula mayai yasiozidi mawili kwa siku na sio vinginevyo. Anasema mwili wa binadamu unahitaji mayai kuongeza protini na Vitamini lakini sio kwa kula mayai mengi kwa siku moja ama kwa wiki. Simwanza anasema mayai ya kware hayana tofauti na mayai ya kuku wa kisasa kutokana na tabia za ufugaji wake.
Anasema wafugaji wengi wanatumia vyakula ambavyo wanawapa kuku wa kisasa kitendo ambacho kinasababisha mayai hayo kutoka kwenye ubora kama yalivyo mayai ya kware ya asili. ‘’Mtu mzima hatakiwi kula mayai zaidi ya mawili hivyo ratiba zinazotolewa na wafanyabiashara hao ni upotoshaji wa makusudi hivyo wanapaswa kuacha mara moja kupotosha umma,’’ anasema Simwanza.
Anaonya kuwa watu wanaokula mayai hayo kwa wingi wana hatari ya kupata magonjwa mbalimbali ya moyo ikiwemo moyo kushindwa kufanyakazi kutokana na wingi wa lehemu zilizopo katika mayai hayo. Anasema pamoja na mambo mengine, mwanadamu anayekula mayai kwa wingi anaweza kupata shinikizo la damu hivyo ni tofauti na wanayoyasema wafanyabiashara.
Anafafanua kuwa ni vyema kwa wananchi kufuata kanuni bora za kula ili kuwa na afya bora na kwamba kufuata wafanyabiashara wasemayo, kutasababisha kuwa na wagonjwa wengi. Hata hivyo, katika baadhi ya taarifa zinaeleza kuwa kula mayai ya kware kwa afya njema, inashauriwa kula yakiwa mabichi. “Watu wengi hawapendi kuyala yakiwa mabichi lakini kuyafanya yawe matamu ni kuchanganya na maziwa na asali.
No comments:
Post a Comment