Sunday 12 July 2015

VIPEPERUSHI VYASAMBAZWA Z`BAR KUPINGA MAAMUZI YA CC KWA KUWAKATAA WANASIASA WAKONGWE BILALI NA EDWARD LOWASSA





Watu wasiofahamika wamesambaza vipeperushi Zanzibar kupinga maamuzi ya Kamati Kuu ya CCM kuwakataa wanasiasa wakongwe waliojitokeza kuwania nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwemo Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilali na Waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa.

Vipeperushi hivyo vyenye kurasa mbili vimeonekana katika maeneo tofauti vikiwa na kichwa cha habari "Sauti ya salama Zanzibar", vimeeleza kuwa kutokana na maamuzi hayo wanachama wa CCM wa kundi la sauti ya salama kuanzia leo ndio mwisho wa wanachama wa sauti ya salama kuendelea kubakia ndani ya CCM.

Walisema kundi hilo linaundwa na mikoa sita ya kichama, wamefikia uamuzi huo baada ya kuridhishwa na utaratibu mzima wa upatikanaji wa mgombea wa nafasi ya urais kutokana na chama kushindwa kupitisha mgombea ambaye ni chaguo la wananchi na wanachama.

“Kama mtatuletea mgombea wenu wa mfukoni badala ya Lowassa ambaye ndio chaguo la wanachama wengi na wananchi, Jumapili ndio mwisho kwa wanachama wa sauti ya salama kuendelea kubakia ndani ya CCM”, vimeonya vipeperushi hivyo.

Aidha, kundi hilo limesema wajumbe wa halmashauri kuu ndio wanaowategemewa na kama watashindwa kukiokoa chama kwa kushindwa kuwapatia wanachotaka, wanachama historia itakuja kuwahukumu kama ilivyotokea kwa vyama vya ukombozi katika mataifa ya Malawi, Zambia na Kenya baada ya vyama husika kushindwa kuheshimu demokrasia ya ndani ya chama.

Kundi hilo limesema kuwa kumbukumbu inaonyesha mchakato wa kupata mgombea wa urais CCM umekuwa ukimalizika na kuacha nyufa ndani ya chama kama ilivyotokea mwaka 2000 baada ya wananchama na wananchi wa Zanzibar kumtaka aliyekuwa Waziri Kiongozi, Dk. Mohammed Gharibu Bilali awe mrithi wa rais mstaafu Dk Salmin Amour, baada ya kumaliza muda wake.

Vipeperushi hivyo ambavyo vimeibua mjadala vimeeleza kwamba mwaka 2010 chama kiliendelea kurejea makosa yale yale kuchagua mgombea wa mfukoni badala ya yule aliyetakiwa na wananchi ambao walikuwa wakimtaka Dk. Bilal na badala yake aliletwa mgombea Dk Ali Mohammed Shein na kusababisha CCM kushinda kwa asilimia 51.

“Kamati kuu, halmashauri kuu pamoja na mkutano mkuu kama utashindwa kusoma alama za nyakati tutalazimika wanachama kupita njia yenye usalama na miguu yetu, kumbukeni vipo vyama vingi na tayari Chadema imetuonesha njia”.

Hata hivyo wasemaji wa CCM hawakuweza kupatikana kutokana na kuhudhuria vikao vya chama Dodoma akiwemo Naibu Katibu mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai, lakini Kamanda wa polisi mkoa wa mjini Magharibi Mkadam Khamis Mkadam, alisema hadi jana hajapokea taarifa ya kusambazwa vipeperushi vinavyopinga maamuzi yanayoendelea kutumika ya kupata mgombea wa urais.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

1 comment:

Anonymous said...



aziz bilal5:24 PM


1
Reply

Imeisha toka hiyo wao walie tuu.

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!