Wednesday, 29 July 2015

UANDIKISHAJI BVR SASA KUANZIA SAA MOJA ASUBUHI

Uandikishaji Dar sasa kuanza saa 1

KATIKA kukabiliana na changamoto ya idadi kubwa ya watu wanaondelea kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mfumo wa BVR jijini Dar es Salaam, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeagiza vituo vya uandikishaji kufunguliwa saa 1 kamili asubuhi.

Awali vituo hivyo vilikuwa vikifunguliwa saa 2 kamili asubuhi na kufungwa saa 12 jioni, lakini kutokana na changamoto ya idadi kubwa ya watu watendaji wa vituo hivyo wameagizwa kuvifungua saa 1 kamili asubuhi ili kuandikisha idadi ya watu zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema, pamoja na changamoto hizo kujitokeza ,wameweza kuandikisha idadi kubwa ya watu na watahakikisha watu wote watakaojitokeza wanaandikishwa na hakuna atakayeachwa.
Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, hadi kufikia juzi idadi ya watu walioandikishwa katika jiji hilo ni 1,172,855 ambapo lengo lao lilikuwa ni kuandikisha watu 2,810,223, hivyo idadi hiyo ni ishara nzuri kuwa watavuka lengo walilojiwekea.
Alisema mashine za BVR zilizoko kwenye vituo ni 3,717 ambapo wilaya ya Ilala yenye vituo 395 ina mashine 927, Kinondoni yenye vituo 702 ina mashine 1462 na Temeke ambayo ina vituo 572 ina mashine 1328. “Baadhi ya changamoto zilizojitokeza zimefanya wananchi kulalamikia mwenendo wa zoezi zima.
Katika kikao ambacho tumekaa na Watendaji wa Manispaa na Mkoa tumeamua kuwa idadi ya waandishi na watendaji katika vituo iongezwe ili kuongeza kasi ya uandikishaji,” alisema Jaji Lubuva.
Aidha, alisema tume hiyo imewaagiza viongozi hao kuwaondoa watendaji wasio na uzoefu katika vituo hivyo ili kuondoa malalamiko ya kuwa na watu wasioweza kutumia vifaa hivyo ambao wanachangia kusababisha msongamano wa watu wakati wa kujiandikisha.
Alisema Tume inakemea vitendo vinavyofanywa na baadhi ya vyama vya siasa na kuvitaka kuacha mara moja kuwachukua wafuasi wao kwenye magari na kuwapeleka katika vituo ambavyo viko katika maeneo ambayo si makazi yao, kwani hilo ni kosa kwa mtu kujiandikisha katika maeneo ambayo si makazi yake.
“Tume inasisitiza wafuasi wa vyama wafuate sheria na taratibu zilizowekwa na si kufanya fujo na ushabiki wa vyama wakati wa uandikishaji. Zipo taarifa kuwa wapo baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa ambao wanaingilia uandikishaji ikiwa ni pamoja na kuzuia uandikishaji kwa baadhi ya wananchi,” alisema.
Aliongeza kuwa vitendo hivyo vinavyofanywa na wanasiasa vimekuwa vikisababisha vurugu na hivyo kusababisha wananchi kukata tama na wengine kuamua kuondoka kwenye vituo hivyo bila kujiandikisha.
Jaji Lubuva aliwataka wananchi kuhakikisha wanapoandikishwa wapewe vitambulisho vyao papo hapo kutokana na kuwepo kwa malalamiko kuwa kuna baadhi ya sehemu wananchi baada ya kuandikishwa wanaambiwa picha watapigwa siku nyingine.
Hata hivyo alisema, wamekuwa wakijitahidi kushughulikia changamoto hizo, licha ya kupokea ujumbe mara kwa mara kupitia simu yake ya malalamiko mengi ya wananchi huku wengine wakimwambia anatakiwa kuwajibika kama alivyowajibishwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Mallaba, ambapo alisema Mallaba hakuwajibishwa ila wakati wake wa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu umefika.

HABARI LEO.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!