Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), inatarajia kuanza kuwasaka viongozi wa umma waliotumia nafasi zao vibaya ikiwamo kuiba na kujilimbikizia mali ndani na nje ya nchi.
Viongozi hao watasakwa na Takukuru kupitia kitengo maalum kilichoanzishwa mwaka jana ambacho kimeanza kupewa mafunzo nchini Uingereza.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah (pichani), aliyasema hayo jijini Dar es Salaam juzi alipokuwa akijibu baadhi ya maswali ya waandishi wa habari.
Dk. Hoseah aliyasema hayo muda mfupi baada ya kufungua mafunzo ya watumishi wa Takukuru ambao wapo katika kitengo hicho ili kuwajengea mbinu na uwezo wa kufanya uchunguzi dhidi ya viongozi walioiba na kujilimbikizia mali.
Alisema kitengo hicho cha Takukuru pia kitakuwa na kazi ya kupambana na masuala ya utakatishaji wa fedha haramu kwa kuwa tatizo hilo linazidi kukua hapa nchini.
Aliongeza kuwa kitengo hicho kilianzishwa rasmi mwaka jana, lakini hakikuanza kazi yake kutokana na kuchelewa kupatikana mtalaam wa kutoa mafunzo kwa watumishi hao.
''Tumejizatiti kukabiliana na viongozi wa umma waliojilimbikizia mali kwa kutumia watalaam wetu ambao wanapatiwa mafunzo," alisema.
Dk. Hoseah alisema huu ni mwanzo na kwamba watahakikisha wanafanya kazi vizuri ili kuwabaini watu walioiba na kujilimbilikizia mali huku akisema kwamba sheria ni msemeno
.
Kuhusu wanasiasa wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, Dk. Hoseah alisema mtu yeyote asithubutu kufanya hivyo kwa kuwa Takukuru imesambaa kila wilaya na kwamba watakamatwa.
''Hawa wagombea wasifanye mchezo mchafu, ninawaonya kwa kuwa tutawakamata popote walipo," alisisitiza.
Aliwaonya wanasiasa wanapita maeneo mbalimbali na kuanza kuchonga barabara na kutoa zawadi nyingine kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa na Takukuru itawashughulikia.
Aliongeza kuwa mtu yeyote atakayepindisha sheria kwamba Takukuru ipo macho muda wote na itawamulika wanasiasa ama wapambe wao ambao watataka kuwahonga wananchi kuwashawishi wawapigie kura.
Hata hivyo, kauli ya Dk. Hoseah imekuwa ya kawaida kutolewa kwa kuwa aliwahi kutangaza vita na wala rushwa wakubwa hapa nchini huku akiahidi kuwaburuza mahakamani, lakini mpaka leo hakufanya hivyo.
No comments:
Post a Comment