Tuesday, 28 July 2015

NI LOWASA VS MAGUFULI


Wakati masikio ya Watanzania yakisubiri nani atateuliwa kuwania urais kupitia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vyama hivyo vimetoa tamko la pamoja la kumkaribisha rasmi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kujiunga na umoja huo.
 
Vyama vinavyounda umoja huo ambao uliasisiwa wakati wa Bunge Maalum la Katiba (BMK) mwaka jana ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (Cuf), NCCR-Mageuzi na National Leaque for Democracy (NLD).
 
Tamko hilo lilitolewa jana na viongozi wakuu wa Ukawa, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia; Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; Mwenyekiti wa Cuf; Prof. Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa NLD, Dk. Emmanuel Makaidi, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya Cuf, Buguruni jijini Dar es Salaam.
 
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Mbatia, akisoma tamko hilo kwa niaba ya viongozi wenzake, alisema uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu, ni fursa ya kipekee ya kuleta mabadiliko makubwa katika nchi ili kuondoa mfumo kandamizi uliopo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 
 “Watanzania wanahitaji mabadiliko yatakayowapatia serikali madhubuti yenye fikra mpya na bunifu kwa maslahi yao, Watanzania wanahitaji mabadiliko yatakayojenga demokrasia ya kweli na kuachana na uonevu, udhalilishaji, fitna na majungu unaoendekezwa na CCM,” alisema.
 
Mbatia alisema hivi sasa Taifa linakabiliwa na ombwe la uongozi ambalo limesababisha nchi kuyumba na kuwa na mipasuko ndani ya jamii na hivyo kuna haja ya kupata uongozi wenye dira, nidhamu na uadilifu utakaolipeleka mbele Taifa.
 
Aliongeza kuwa uchaguzi wa mwaka huu ukitumiwa vizuri na kimkakati, utaleta mabadiliko makubwa yanayotakiwa na wananchi na kwamba Ukawa wanaamini katika kuweka mbele maslahi mapana ya wananchi kwa kujenga mshikamano ndani na nje ya vyama.
 
MCHAKATO URAIS CCM ULIKIUKA KANUNI
Mbatia akizungumzia mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya CCM, alisema Watanzania wameshuhudia hadaa, uonevu, udhalilishaji, upendeleo na ukandamizaji.
 
Alisema mchakato huo ambao ulimpa ushindi Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kuteuliwa na CCM kuwa mgombea urais, ulitawaliwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu, kanuni na katiba ya chama hicho.
 
SIFA ZA VIONGOZI
“Katika kutafakari kwa kina maslahi mapana ya Taifa letu, Ukawa tunahitaji viongozi wenye sifa, uwezo na weledi katika kulinda, kuheshimu na kusimamia rasilimali za Taifa kwa maslahi ya Taifa,” alisema .
 
Mbatia aliongeza kuwa viongozi wenye sifa hizo hawawezi kuwa ndani ya CCM kwa sababu mfumo wa chama hicho tawala haumpi kiongozi binafsi kutumia vipaji vyake au ubunifu katika kusimamia maslahi ya Taifa.
 
Alisema Ukawa unaamini ili kuwa na maslahi mapana ya Taifa, anahitajika Mtanzania ambaye yupo tayari kujiunga na Ukawa kuhakikisha Taifa linakuwa salama na lenye amani ya kweli ambayo msingi wake ni haki.
 
WAMKARIBISHA LOWASSA
“Tunachukua fursa hii ya kipekee kumwalika Waziri Mkuu mstaafu na Mbunge wa Monduli, Lowassa, ajiunge na Ukawa na tuko tayari kushirikiana naye katika kuhakikisha kuwa tunaiondoa CCM madarakani katika uchaguzi mkuu ujao,” alisema Mbatia.
 
Alisema Ukawa inamkaribisha Lowassa kwa sababu ana uwezo wa kuhamasisha umma kuikataa CCM yenye kusimamia mifumo isiyotenda haki na ni mchapakazi makini na mfuatiliaji wa karibu wa utendaji katika majukumu anayokabidhiwa.
 
“Ni rai ya Ukawa kwa kila Mtanzania ambaye yupo tayari kuuondoa mfumo huo kandamizi na dhalimu wa CCM kushirikiana na Ukawa kwa lengo la kujenga Taifa imara, Ukawa ndilo tumaini la Watanzania, tusikubali kunyamaza pale sauti zetu zinaponyamazishwa kwa lazima na bila sababu, tusikubali kunyimwa fursa ambazo tuna uwezo nazo, tuwe tayari kushiriki michakato ya kidemokrasia ya kuleta mabadiliko na kupata viongozi bora,” alisema.
 
Alisema Ukawa katika uchaguzi wa mwaka huu itaweka mgombea mmoja wa udiwani katika kila kata na wadi, mgombea mmoja wa ubunge na uwakilishi kwa kila jimbo na mgombea mmoja wa urais wa Zanzibar na mgombea mmoja wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
LOWASSA SIYO FISADI
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Mwenyekiti wa NLD, Dk. Makaidi alisema Lowassa ni mtu safi na siyo fisadi kama inavyoelezwa na ndiyo maana yupo uraiani, hayupo jela.
 
“Tunaamini Lowassa ni mtu safi na ndiyo maana yupo hadi sasa hayupo jela, mafisadi wapo jela, Lowassa tunamkubali,” alisema.
 
Naye Mwenyekiti wa CUF, Prof. Lipumba alisema suala la ufisadi ni suala la mfumo uliopo ndani ya CCM na mfumo huo ndiyo unaoleta ufisadi.
 
“Lowassa alijiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008, tujiulize tangu amejiuzulu je, ufisadi umepungua au umeongezeka ndani ya serikali ya CCM, kimsingi hili suala la kimfumo tu ndilo linasababisha ufisadi ndani ya CCM,” alisema.
 
Naye Mbatia akijibu swali la kwamba inakuwaje leo hii vyama hivyo vimuone Lowassa mtu safi wakati vilikuwa vikimtangaza ni fisadi, alisema kwenye siasa kila chama kilichosajiliwa ni chama pinzani dhidi ya kingine.
 
Alisema kusudio la Ukawa ni sauti ya Watanzania kupigania Katiba mpya. 
 
“Chadema kinaweza kuwa mpinzani wa Cuf, NCCR-Mageuzi inaweza kuwa mpinzani wa NLD, Cuf inaweza kuwa mpinzani wa NCCR-Mageuzi,” alisema.
 
MGOMBEA URAIS UKAWA AGOSTI
Viongozi hao wa Ukawa wakijibu swali kama Lowassa atakapojiunga na umoja huo watamteua kuwa mgombea urais wao, Prof. Lipumba alisema suala la kumtangaza mgombea urais ni lazima lifuate taratibu na kanuni za kila chama.
 
Alisema mgombea urais Ukawa kupeperusha bendera yao atajulikana rasmi mwanzoni wa mwezi ujao.
Naye Mbatia alisema wakati wa kumtangaza mgombea urais Ukawa, zitafanyika sherehe kubwa na kwamba Watanzania wasubiri atapatikana mgombea mzuri.
 
Hata hivyo, viongozi hao wa Ukawa hawakuweka wazi kama Lowassa atajiunga na chama gani kati ya vinavyounda umoja huo na kama atateuliwa kugombea urais baada ya kujiunga na Ukawa.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!