Friday, 17 July 2015

Nchi 21 zaunga mkono mikakati kudhibiti ebola.



Nchi 21 ambazo zilichangia mapambano dhidi ya ugonjwa wa ebola zimeunga mkono mikakati iliyowekwa na jopo la kimataifa linalopendekeza jinsi dunia inavyoweza kukabiliana na majanga yajayo ya magonjwa ya milipuko.



 
Mwenyekiti wa jopo hilo ni Rais Jakaya Kikwete (pichani) ambaye Julai 15, mwaka huu aliongoza mkutano wa nchi hizo katika makao ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini Geneva, Uswisi na nchi hizo kuunga mkono kazi inayofanywa na jopo hilo. 
 
Nchi zilizounga mkono ni  Venezuela, Umoja wa Ulaya (EU), Uholanzi, Finland, Russia, Norway, China, Ubelgiji, India, Ujerumani, Marekani, Uswisi, Canada, Brazil, Denmark, Uingereza, Israel, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Umoja wa Afrika (AU), Benki ya Dunia (WB), Jamhuri ya Korea na Japan.
 
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, pamoja na kwamba wajibu mkuu wa jopo hilo siyo kuchunguza ugonjwa wa ebola na madhara yake, bado ugonjwa huo ni msingi mkuu wa kazi ya jopo hilo ambalo wajibu wake ni kutumia uzoefu wa ebola kutoa mapendekezo ya jinsi dunia inavyoweza kukabiliana na majanga ya magonjwa ya milipuko katika siku zijazo.
 
Ugonjwa wa ebola ambao ulilipuka katika nchi hizo tatu za Afrika Magharibi mwishoni mwa mwaka 2013 mpaka sasa umeua watu 11,000 katika nchi hizo.
 
Hiyo ilikuwa mara ya 24 kwa ugonjwa huo kulipuka katika Afrika. Mara ya kwanza ulipolipuka mwaka 1976 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wakati huo ikiitwa Zaire. 
 
Taarifa hiyo imesema jopo hilo liliambiwa kuwa tofauti na matarajio ya dunia kuwa ugonjwa huo ulikuwa umedhibitiwa katika nchi hizo hasa Liberia, lakini umeanza kupata kasi tena katika nchi hizo tatu na zinakisiwa kuwa na wagonjwa karibu 70.
 
Jopo hilo lenye wajumbe sita liliteuliwa Aprili, mwaka huu, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon.
 
Taarifa imesema Rais Kikwete na jopo lake walimepata nafasi ya kumsikiliza aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, wakati ugonjwa huo unalipuka Dk. Luis Gomes Sambo wa Angola ambaye aliwaeleza historia ya ofisi ya kanda hiyo iliyoko mjini Brazzaville, Jamhuri ya Congo, katika kukabiliana na ugonjwa huo.
 
Walielezwa na Mkurugenzi mpya wa Kanda, Dk. Matshidizo Rebecca Moeti ambaye amezungumza kwa njia ya mkutano mtandao kutoka mjini Brazzaville.
 
Wajumbe walipata fursa ya kusikiliza jitihada za Rwanda kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kupitia kwa Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Agnes Binagwaho, ambaye naye alizungumza kwa mtandao kutoka Rwanda. 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!