Monday, 27 July 2015

MKUYA: HATUTAPUNGUZA USHURU WA KUINGIZA MABASI NCHINI


Serikali imesisitiza kuwa haitaweza kupunguza ushuru wa uingizaji wa mabasi nchini kutoka asilimia 25 hadi 10  kwa kuwa hayo yalikuwa makubaliano ya nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

 
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alisema hayo wakati akizungumza na NIPASHE kupata msimamo wa Serikali kufuatia wamiliki wa mabasi nchini kuitaka ipunguze ushuru huo ama kinyume chake wataitisha  mgomo nchi nzima.
 
Mkuya alisema Serikali ya Tanzania iliiomba EAC kupunguza kodi kufikia asilimia 10 kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo kasi kwa ajili ya jiji la Dar es Saalam, makubaliano ambayo yaliishia Juni mwaka huu.
 
 “Waagizaji wa mabasi walikuwa na muda wa mwaka mzima wa kuagiza magari kwa kutumia ushuru wa asilimia 10 ambao Tanzania iliiomba jumuiya kuipunguzia ulioishia Juni mosi mwaka huu,” alisema.
 
Alisema baada ya kipindi hicho kumalizika  hakuna namna yoyote ambayo Serikali kufanya kwani hayo ni  makubaliano ya nchi wanachama na sio makubaliano ya Serikali.
 
 Hata hivyo, Waziri Mkuya alikanusha madai ya kuwa kuna msamaha wa ushuru kwa waingizaji wa maroli nchini na kusisitiza kuwa  hakuna msamaha kwa waingizaji hao kama ilivyodaiwa na baadhi ya wamailiki wa mabasi kupitia mkutano wao, isipokuwa Serikali imefuta ushuru kwa viwanda vya ndani vinavyounganisha maroli hayo.
 
Naye Katibu Mkuu wa wamiliki wa mabasi Tanzania (Taboa), Enea Mrutu, alisema msimamo huo wa serikali utasababisha kusimama kwa huduma.
 
Alisema Serikali ingetumia ushuru wa asilimia 10 ili wafanyabiashara waweze kuyaondoa mabasi yao yaliokwama bandarini kutokana na gharama kubwa za uingizaji wa mabasi kupandishwa gafla.
 
“Bandarini kuna mabasi zaidi ya 44 kutoka China ambayo yaliingia nchi kati ya Julai Mosi hadi 10 ambayo yamekwama kutokana na kutozwa ushuru mkubwa, serikali ingetushirikisha toka awali haya yote yasingetokea,”alisema.
 
Tabao walifanya mkutano mkuu uliokuwa na majadiliano kuhusu kupanda kwa gharama za ushuru wa uingizaji wa mabasi nchini ambao walikubaliana kuwa endapo Serikali isiposhusha gharama hizo wataitisha mgomo nchi nzima.
 
Katika mkutano huo walikubaliana kuunda kamati ya watu watano itakayoonana na Waziri wa Uchukuzi na Waziri wa Fedha kwa lengo la kujadiliana kupanda kwa gharama za ushuru wa uingizaji wa mabasi nchini. 

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!