Sunday, 12 July 2015

MENGI ZAIDI JUU YA MHINDI ALIYEKUTWA HOTELINI NA MABEGI YALIYOJAA PESA DODOMA



Ilikuwa kama sinema wakati mabegi matatu yaliyokuwa yamesheni mamilioni ya fedha yalipokamatwa katika hoteli ya St. Gaspar mjini hapa, fedha zinazodaiwa kuwa zimetolewa na Mfanyabiashara Yusufu Manji, kwa nia ya kuhonga wajumbe wa vikao vya maamuzi vya Chama Cha Mapinduzi (CCM).



Fedha hizo zilikamatwa jana katika hoteli hiyo iliyopo eneo la Kisasa, zikiwa mikononi mwa mfanyakazi wa Kampuni ya Quality Group (T), Amit Kevaramani, akiwa na hati ya kusafiria M1470774 ya nchini India.
 Quality Group (T) inamilikiwa na Yusuf Manji.

Kiasi cha fedha kilichokamatwa hakijaweza kuthibitika mara moja, ila waliohusika katika kamata hiyo na baadaye kushuhudia polisi waliofika eneo la tukio baada ya kuitwa kuhesabu, walisema zinafikia Sh. 725,2050,000.

Mbali na polisi, maofisa wengine wa vyombo vya usalama walioshuhudia rundo hilo la fedha za noti za Sh. 5,000 na 10,000 zikiwa zimefungwa kwa mabunda ya Sh. milioni 10 kila moja, ni maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Usalama wa Taifa.

Waliomkamata na fedha hizo walishtukia mwenendo wa mfanyakazi huyo, aliyeonekana akihamisha mabegi makubwa moja baada ya jingine kupeleka kwenye gari lililokuwa limeegeshwa nje ya hoteli hiyo likiwa na namba za usajili T687 ANQ Toyota Land Cruiser.

Katika hoteli hiyo ambayo kulikuwa na wajumbe wengi wa Mkutano Mkuu, na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM inadaiwa kuwa mamilioni hayo yalikuwa yanapelekwa kwa kambi ya mmoja wa wagombea watano waliopitishwa na Kamati Kuu, juzi usiku.

Katika simu ya mkononi ya mtuhumiwa huyo, ilipokaguliwa na waliomkamata zilikutwa jumbe fupi za maandishi (SMS) zilizotumwa kwake kutoka kwa mfanyabiashara (Manji) zikimueleza watu wa kuwapeleka fedha hizo.

Mfanyakazi huyo akizungumza kwa Kiingereza na Kiswahili cha kubabaisha, alipogundua kuwa amekamatwa, alijaribu kumhonga mwanamke mmoja begi moja lenye fedha, lakini alikataa na kuwaita watu wengine kushuhudia tukio hilo.

Katika simu yake, miongoni mwa waliotakiwa kupewa fedha ni Mbunge mmoja wa jimbo lililopo Dar es Salam ambaye alitakiwa kupewa milioni 10 kama mkopo na alitakiwa asaini vocha ya malipo.

Wengine walionufaika na mgawo huo, ni manaibu waziri wawili, mmoja milioni 15 na mwingine milioni 10.

Aidha, kwenye simu hiyo kulikuwa na orodha ndefu ya watu waliotakiwa kupewa fedha hizo.

Mbali na mfanyabiashara huyo kukamatwa na polisi, dereva kutoka kampuni ya Ngatuni Traders, Rashid Nkungu, ambaye alikodishwa na mfanyakazi wa Manji, aliwaambia waandishi wa habari kuwa alitumwa kwenda kuwapokea katika uwanja wa ndege wa Dodoma juzi asubuhi majira ya saa 1:30.

Alisema mfanyakazi huyo alikuwa amefuatana na wenzake watatu, wote wenye asilia ya Asia.

“Mimi hawa Wahindi wamekodisha gari katika ofisi yetu, mimi ni dereva nimewapokea uwanja wa ndege nikawaleta hapa St. Gaspar, walikuwa na mabegi yao kutoka uwanja wa ndege mpaka hapa walikuwa wanne,” alisema Nkungu.

Aidha, alisema kati ya abiria hao wanne, aliweza kumtambua mmoja wao ambaye ni Yusuph Manji na baadaye aliwatoa hotelini hapo na kuelekea Benki ya CRDB tawi la Dodoma.

Alisema aliwapeleka benki watatu na baadaye akawarudia wawili mmoja wao akabaki benki.

Walipofika hotelini abiria hao walimchukua mwenzao mmoja kisha wakaelekea uwanja wa ndege Dodoma.

 “Hakuna Mswahili hata mmoja aliyekuja kuwapokea wote walikuwa Wahindi na hakuna mtu aliyekuja kuwapokea zaidi yangu mimi, kuna mmoja nilimtambua ambaye ni Manji,” alisema Nkungu.

Alisema baada ya kuwapeleka uwanja wa ndege, Nkungu alisema kuwa alipita benki kumchukua aliyebaki huko, alitakiwa aingize gari kwenye uzio wa benki, kisha alitoka mfanyakazi huo akiwa na begi.

“Baada ya kuwarudisha hapa nikalipwa hela kiasi cha Shilingi laki tatu nikaondoka, kurudi zangu nyumbani na tukaagana vizuri na leo asubuhi (jana) akanipigia tena nimfuate nimpeleke airport namba yake sikuwa nakumbuka  inaishia namba 24,” alisema Nkungu.

Hata hivyo, alisema baada ya kufika na kumsubiri nje mfanyakazi huyo alitoka na kupakia kwenye gari begi la kwanza na kumtaka dereva huyo asikae ndani ya gari na pia akarudi kupakia begi la pili na kumwambia aendelee kusubiri nje, lakini baadaye akaona mtu anakuja na kupiga picha gari mbele na kuchukua ufunguo na kuzima gari.

Kwa upande wake, Meneja wa Hoteli hiyo, Denis Johannes, alisema mgeni huyo alipokelewa juzi katika hoteli hiyo akidai kuwa alitumwa na ubalozi wa India na kulazimika kumpatia chumba kimoja.

“Sisi kama hoteli mgeni tunamsikiliza na tuna uhusiano mzuri sana balozi zote Tanzania, Balozi yeyote yule akikosa nafasi tunampa kipaumbele, na walipoingia walisema wao wametumwa na  balozi ya India, na kuangalia alivyo walisema wamekosa vyumba katika hoteli ya Moreno wakasema kwa hiyo wamekuja hapa,” alisema Meneja huyo.

Alisema awali aliwajibu kuwa hana taarifa za kuwapo kwa chumba kwa ajili yao, lakini kwa kuzingatia ushirikiano na balozi zilizopo wakaamua kumpatia chumba kimoja.

Hata hivyo, baada ya kukagua nyaraka za kujisajili kulala hotelini hapo, aligundua kuwa maelezo binafsi ya mteja huyo ni tofauti na alivyojieleza awali.

*Imeandikwa na Godfrey Mushi, Editha Majura, Jacqueline Massano na Agusta Njonji, Dodoma

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!