Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, leo atachukua fomu ya kuomba ridhaa ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salim Mwalimu, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana alisema Lowassa, ambaye alijiunga na Chadema juzi, atachukua fomu hiyo saa 5:00 asubuhi makao makuu ya Chadema Kinondoni.
“Mengine ni hiari ya mgombea kama atakuja na watu, mwenyewe, mbwembwe zozote anazotaka atafanya ni hiari ya mgombea, lakini muda huo ndiyo atachukua fomu ya urais,” alifafanua.
Lowassa ni Mbunge wa Monduli, pia alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka miwili katika Serikali ya Awamu ya Nne.
Katika hatua nyingine, aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, James Ole Medeye, jana alikuwapo kwenye mkutano huo akiwa amekaa mstari wa mbele wa viongozi wa chama hicho.
Alipoulizwa na waandishi juu ya uwapo wake katika makao makuu ya Chadema, alisema alikuwa mpita njia akakaribishwa kwenye ofisi ya umma.
“Hii ni ofisi ya umma ya chama kinachohudumia umma wa Watanzania, wamenikaribisha nami nimeamua kuja kushiriki nao, mimi bado ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi, nimeamua kushirikiana nao kwa kuwa kazi wanayoifanya ni ya umma wa Watanzania,” alisema Medeye ambaye ni Mbunge wa Arumeru Magharibi kwa tiketi ya CCM.
Huku akishindwa kueleza moja kwa moja kama ameshajiunga na Chadema na kukabidhiwa kadi, alisema wakati ukifika atasema lakini kwa sasa bado ni mwanachama hai na hakuna kipengele kwenye Katiba ya CCM kinachokataza mwanachama wake kutembea kwenye ofisi za vyama vingine.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Gologwa, alisema Medeye na wenzake watapokelewa mkoani Arusha katika mkutano mkubwa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
“Hadi sasa sijamkabidhi kadi lakini ni mwenzetu ndani ya chama na wakati wowote atakamilisha taratibu za kuwa mwanachama rasmi, wapo wengine tutaendelea kuwapokea na wote watapokelewa jijini Arusha,” alisema.
WENGI WAMFUATA LOWASSA
Mkoani Mtwara, wanachama 63 wa CCM, kata ya Dihimba wamerudisha kadi zao na kujiunga na chama hiyo kwa madai ya kutoridhishwa na chama hicho kwa kushindwa kutenda haki wakati wa mchakato wa mgombea urais ndani ya chama mwanzoni mwa Julai, mwaka huu.
Akizungumza na NIPASHE jana, Katibu wa Chadema Wilaya ya Mtwara Vijijini, Patrick Simwinga, alisema wanachama hao walijiunga baada ya kuwa na vikao vyao vya ndani kwa muda mrefu.
“Jana tulikuwa na vikao vya ndani vya chama baada ya kikao hicho nje ya ukumbi huo nilikutana na kundi la watu waliomba kuhamia katika chama chetu huku wakisema kama CCM imeshindwa kumtendea haki Lowassa sisi tutakuwa katika hali gani,” alisema.
Aidha, alisema kutokana na Lowassa kuwa na wafuasi wengi na mvuto kwa watu, chama hicho kinategemea kuvuna wanachama wengi zaidi na kueleza kuwa baadhi ya viongozi wakubwa wanamuunga mkono Lowassa.
“Kuna viongozi wengi ambao tunawafahamu wameahidi kumuunga mkono Lowassa na kujiunga na chama chetu, mafuriko ni makubwa ya wanachama wa CCM ambao wamekatishwa tamaa na mfumo kandamizi na sisi tunatarajia kupokea wanachama wengi na hii ndiyo furaha yetu sisi kama chama maana lengo letu ni kupata wanachama wengi,” alisema Simwinga bila kutaja majina ya wanachama hao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Rasilimali Chadema, Mustafa Atengikwe, alisema vijana wa Mtwara Mjini wamekuwa wakijitokeza kuomba kadi kujiunga na chama hicho.
“Leo asubuhi, kuna vijana wamefika hapa ofisini wakiomba kadi kwa ajili ya kujiunga na chama chetu, lakini nimeshindwa kutokana na ukweli kwamba tumeishiwa kadi,” alisema Atengikwe.
Said Hassan (34), mkazi wa Ligula, alisema wakati umefika kwa vijana kuhakikisha wanatumia nafasi yao kwa ajili ya kuchagua kiongozi ambaye anachukia umaskini.
WANA-CCM 54 DODOMA WATIMKIA CHADEMA
Wana-CCM 54, akiwamo Mwenyekiti wa tawi la Mlimwa Kusini, kata ya Ipagala Wilaya ya Dodoma Mjini, Yahaya Said, wametimkia Chadema.
Akizungumza wakati akiwapokea wanachama hao, Katibu wa Chadema wa wilaya hiyo, Vincent Emmanuel, alisema watawapa ushirikishiano wa kutosha wanachama wote wapya wanaojiunga na chama hicho.
“Mwenyekiti wa tawi, amejiunga na chama chetu na kuomba kugombea udiwani katika kata ya Ipagala,” alisema.
Alisema watu watano wametia nia ya kuwania udiwani katika kata hiyo.
Kwa upande wake, Said alisema ameamua kuondoka CCM kutokana na ubabaishaji na chama kuonekana kama ni mali ya mtu binafsi.
“Tukiangalia kwenye Bunge, wabunge wanaotetea maslahi ya wananchi ni kutoka upinzani na wabunge wa CCM wamekuwa wakitetea maovu tu na ndiyo maana tumeamua kuhama,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (Cuf) kata ya Ipagala, Ismail Seif, alisema hayo ni matunda mazuri ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema kata ya Ipagala, Jella Mambo, alisema kura za maoni za wagombea udiwani zitafanyika leo na kesho katika kata zote mkoani humu.
LISSU, MWALIMU WAZUNGUMZIA UZUSHI
Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, alisema taarifa zinazosambaa kuwa amekihama chama hicho hazina ukweli na kwamba Julai 27, mwaka huu, aliandika kwenye ukurasa wake wa facebook kuhusu Lowassa kujiunga na Ukawa na kuwa anafaa kuwa mgombea urais.
Lissu ambaye katika Bunge la 10, alikuwa Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni, alisema Lowassa hakuwekwa kwenye orodha ya mafisadi kwa kuwa suala lililojadiliwa na kutolewa uamuzi ni Richmond, ambalo katika maelezo yake juzi alieleza kwa uwazi kuwa lilifanyika kwa maelekezo ya uongozi wa juu wa nchi.
“Kama wapo watakaojiondoa pia wengi watakuja, tupo katika kipindi ambacho Taifa halijawahi kukipita tangu Uhuru, mfumo tawala unabomoka vipande vipande na dalili kubwa ni viongozi wa juu kujiunga na Chadema,” alisema.
Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki aliyemaliza muda wake, alisema mapinduzi ya nchi yanatokea pale mfumo tawala unapopasuka.
"Tumeongeza nguvu katika mabadiliko na katika mabadiliko ni lazima mfumo uvunjike vipande vipande hadi vumbi linalotimka sasa litulie mfumo tawala utakuwa umeanguka," alisisitiza.
“Hakuna maamuzi yaliyofanywa ndani ya Chadema bila kuwashirikisha viongozi wakuu wa chama, wamehusika katika hatua zote,” alifafanua Lissu.
Kuhusu tetesi za mtandaoni kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, kujiunga na CCM kwa madai ya kutofurahishwa na Lowassa kujiunga na Chadema, Mwalimu alisema hazina ukweli wowote.
Mwalimu alisema Dk. Slaa na Naibu Katibu Mkuu, John Mnyika, wako katika shughuli za ujenzi wa chama.
“Kipindi cha uchaguzi kuna mambo mengi, mikakati ni mingi, wapo wengine wapo mikoani wanaendelea kuimarisha chama, Dk. Slaa yupo katika majukumu mengine na siyo kila tukio wote wawepo,” alifafanua.
Imeandikwa na Salome Kitomari (Dar), Mariam Maregesi (Mtwara) na Jacqueline Massano (Dodoma)
No comments:
Post a Comment