Waziri Mkuu wa Australia, Tony Abbot, amempongeza Rais Jakaya Kikwete, kwa kuamua kukabidhi madaraka kwa kiongozi mwingine kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania.'
“Nakupongeza sana kwa uamuzi wako wa kukabidhi madaraka kwa amani nchini kwako, ni jambo la nadra sana barani Afrika, kuwa na utaratibu mzuri na wa amani namna hii," Abbot alimuambia Rais Kikwete.
Aliongeza: "Australia itaendelea kuisaidia Tanzania katika juhudi zake za kuleta maendeleo na kukuza uchumi."
Rais Kikwete na Waziri Mkuu Abbot, pia walizungumzia jinsi nchi zao zinavyoweza kuendelea kushirikiana katika kulinda usalama baharini, kukuza zaidi ushirikiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii.
Rais Kikwete yuko nchini Australia kwa mwaliko wa kiserikali kutoka kwa Gavana Mkuu wa Australia, Peter Cosgrove.
Ushirikiano wa Tanzania na Australia umedumu tangu miaka ya 1960 na sasa nchi zimeazimia kuimarisha uhusiano zaidi katika sekta mbalimbali zikiwamo za uwekezaji na biashara.
Jana Rais Kikwete alitarajiwa kukutana na wawekezaji wakubwa wa Australia ambao tayari wanawekeza nchini kwa ajili ya mazungumzo kuhusu namna ya kuendeleza sekta mpya ya gesi nchini na jinsi Tanzania itakavyonufaika kutokana na kupata nishati hiyo.
Tayari Serikali ya Australia na kampuni binafsi za gesi na mafuta, zinaisaidia Tanzania hasa katika vyuo vya ufundi stadi (Veta) na tafiti mbalimbali katika kilimo.
Leo Rais Kikwete anatarajia kutunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Newcastle, kwa mchango wake mkubwa alioutoa katika uongozi kwa kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake nchini na dunia kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment