Wilaya za Kilwa, mkoani Lindi na Geita, mkoani Geita, zimeelekeza fedha za gesi na madini kwenye ‘ulaji’ zaidi kuliko miradi ya maendeleo na uwekezaji wenye manufaa kwa wananchi wote.
Kadhalika, Halmashauri zilizofanyiwa utafiti ikiwamo ya Tarime zimeshindwa kuwa na uwekezaji wa kudumu unaotokana na fedha hizo, kwa ajili ya miaka mingi ijayo baada ya raslimali hizo kwisha.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na kamati ya kudumu ya viongozi wa dini inayojihusisha na uchumi, haki na uhifadhi wa uumbaji, katika wilaya za Geita, Kilwa na Tarime, fedha hizo hazijatumika kuwekeza kwenye miradi yenye manufaa baada ya rasilimali husika kwisha.
Kamati hiyo inajumuisha Baraza la Waislmu Tanzania, Baraza la Makanisa ya Kikiristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC).
Mtafiti Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prosper Ngowi, akiwasilisha utafiti huo kwa viongozi wa dini na serikali kwa Wizara za Nishati na Madini, Fedha na Tamisemi, alisema wilaya ya Tarime ndiyo ilielekeza fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo na ina kampuni za wazawa zinazotoa huduma kwenye kampuni za uchimbaji.
Alisema makubaliano yaliyokuwepo kabla ya sheria mpya, kampuni zinazjihusisha na uchimbaji zinapaswa kuchangia Dola za Marekani 200,000 na kwa sasa ni asilimia 0.3 ya pato ghafi kwa halmashauri husika.
Alisema asilimia 91.2 ya fedha walizopata kutoka kampuni ya Pan Africa Energy zilielekezwa kwenye matumizi ya kawaida ambayo ni kugharamia vikao, posho na semina huku miradi ya maendeleo zikipelekwa asilimia 8.2.
Alisema Halmashauri ya Tarime ndiyo ilitenga fedha hizo asilimia 45 kwa miradi ya maendeleo na asilimia 55 matumizi ya kawaida.
Alisema Halmashauri ya Geita yenye migodi mitatu inayomilikiwa na kampuni ya Acacia, asilimia 72 zilielekezwa kwenye matumizi ya kawaida na asilimia 28 miradi ya maendeleo.
“Haiwezekani fedha nyingi tunazielekeza kwenye ulaji zaidi na kiduchu ndizo za maendeleo ya watu wengi,” alisema.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora, Paul Ruzoka, alisema walipoitembelea maeneo yenye utajiri huo wamebaini kuwa wananchi wana hali duni ya maisha tofauti na kipato kinachotokana na utajiri kwenye eneo lao.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment