Watanzania wanaoishi nje ya nchi wamesema wangependa serikali ijayo iendeleze jitihada za kuimarisha uchumi kuanzia atakapoishia Rais Jakaya Kikwete.
Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Uholanzi (TANE) walimueleza Rais Jakaya Kikwete katika risala yao iliyosomwa na Makamu Mwenyekiti wa Mpito, Johannes Rwanzo, baada ya Rais kuzungumza na Watanzania hao jioni juzi jioni, mjini hapa.
"Tunaomba serikali ijayo iendeleze pale utakapoishia, Tunajua kuna mambo mengi ambayo labda muda wa awamu mbili hautoshi kuyakamilisha, basi tungeomba mambo haya uyakabidhi kwenye utawala unaofuata ili waendeleze pale utakapokuwa umefikia,” alisema
Rwanzo aliyataja baadhi ya mambo ambayo yanahitajika kuendelezwa na awamu ijayo kuwa ni pamoja na juhudi za kupambana na umaskini nchini na ujenzi wa miundombinu.
Watanzania hao pia walimuomba Rais Kikwete kuwa pamoja na kustaafu, bado wangependa aendelee kutoa msaada kwa wananchi wa Tanzania kwa kuwa kustaafu sio mwisho wa kusaidia jamii.
Rais Kikwete alikuwa katika ziara ya kikazi ya kuishukuru Uholanzi kwa misaada ya kimaendeleo na pia kuiomba iendelee kuisaidia Tanzania ili kukamilisha na kuendeleza juhudi za kujenga na kuimarisha uchumi kwa nia ya kuleta maendeleo Tanzania.
Rais Kikwete aliwaeleza Watanzania kuhusu uchaguzi mkuu ujao ambao aliahidi kuwa utasimamiwa vizuri ili Watanzania wapate nafasi ya kuchagua viongozi wanaowataka.
No comments:
Post a Comment