Tuesday, 9 June 2015

WATANZANIA MILIONI 21 WAPATA ZAIDI YA DOZI MILIONI 52 ZA DAWA ZINAZOTIBU MAGONJWA YASIYOPEWA KIPAUMBELE

Zaidi ya dozi milioni52 za dawa zinazotibia magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ya matende, vikope, mabusha,minyoo ya tumbo, kichocho na usubi zimetolewa na Serikali kwa watanzania milioni 21 katika kipindi cha mwaka 2014.


Takwimu hizo zimetolewa jana jijini hapa na Katibu Mkuu wizara ya Afya na ustawi wa jamii Dkt Donan Mmbando katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa nne wa kazi kati ya wizara hiyo na wadau wanaofadhili mpango huo iliyosomwa kwa niaba yake na mkurugenzi wa idara ya huduma ya kinga katika wizara hiyo Dkt.Neema Rusibamayila.
Dkt. Rusibamayila alisema katika kipindi cha mwaka 2014/2015, mpango huo ulifanikiwa kuwafikia watanzania katika wilaya 110 na mikoa 17 ya Tanzania ikiwemo wanafunzi katika ngazi za shule ya msingi na watoto wenye umri wa kwenda shule.
Hata hivyo alisema katika kwa mwaka huu mikoa minne zaidi inayokabiliwa na tatizo la magonjwa hayo imelazimika kuongeza idadi ya mikoa katika mpango huo ikiwemo mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Simiyu, , Geita .
“Leo ikiwa tunakutana hapa tunajivunia kazi tuliyoifanya kwa kuwa tayari Takwimu zinaonyesha wilaya 6 hazihitaji dawa za matende ugonjwa huo umeshamalizika, ugonjwa wa trakoma tulifanya utafiti wa awali wilaya31 tumegundua ni wilaya moja tu ya Chunya Mkoani mbeya ndio imekuwa ikihitaji dawa ,Vilevile thathmini ya trachoma iliyofanyika katika wilaya 28 imeonyesha kuwa wilaya 19 zimefaulu hivyo kutohitaji ugawaji dawa wakati 9 zitaendelea na ugawahji dawa za Zithromax,”alisema.
Kwa upande wake Mratibu wa Taifa wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kutoka wizara ya Afya na ustawi wa jamii Dkt. Upendo Mwingira alisema mpango huo wa Serikali umekuwa na faida nyingi kuliko changamoto.
“Baadhi ya changamoto ni pamoja na utoaji huduma kwa wagonjwa wanaohitaji upasuaji hasa kwa wale ambao wamekwisha athirika na magonjwa haya hasa vikope na matende, tunawasiliana na wadau wetu ili kuwapatia huduma hii, lakini pia kuna tatizo la uelewa ijapokuwa wengi wamekuwa waelewa baada ya kutumia mbinu mbalimbali za kuwaelimisha umuhimu wa zoezi tunalokuwa tunafanya,”alisema.
Kwa upande wake Kaimu mganga mkuu wa Mikoa wa Arusha Dkt. Omar Chande, alisema zoezi la ugawaji wa dawa za kuzuia maambukizi ya magonjwa hayo limeenda vizuri na matokeo yanaonyesha zaidi ya asilimia 85 ya watoto wenye umri wa kwenda shule walipata dawa za kichocho na minyoo mnamo mwezi Mei 2015. utafiti wa awali umeonyesha kuwa wilaya zote zimeathiriwa na baadhi ya magonjwa hayo.
Alisema Mkoa wa Arusha unajipanga kutoa tiba ya upasuaji wa ugonjwa wa trakoma kwa wakazi wa wilaya za Longido na Monduli sanjari na kuendelea na zoezi la ugawaji wa dawa kwa wilaya zingine tatu Julai mwaka huu.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!