Wabunge wameitupia lawama Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushindwa kutekeleza utaratibu wa utoaji matibabu bure kwa wazee, hali ambayo imesababisha wakabiliwe na hali ngumu ya maisha na wengine kupoteza maisha wao kwa kukosa huduma za matibabu.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Raya Ibrahim Hamis, alisema licha ya kuwapo kwa sera ya inayotoa maelekezo kwa wazee kutibiwa bure, lakini jambo hilo limekuwa kiini macho kutokana na wazee kunyimwa matibabu.
Alisema wazee wanapokwenda katika hospitali, vituo vya afya na zahanati kwa ajili ya kutibiwa wakishapewa vipimo wanaambiwa wakanunue dawa katika maduka ya dawa.
Naye Mbunge wa Kibaha Mjini (CCM), Silvester Koka, alisema Wazee wametelekezwa katika matibabu kila wanapokwenda katika dirisha maalum kwa ajili kupewa matibabu wakati mwingine wamekuwa wakinyimwa huduma hiyo.
Koka aliitaka serikali kuiboresha Hospitali ya Tumbi kutokana na umuhimu wake wa kupokea wagonjwa wanaopata ajali katika barabara Kuu ya Dar es Salaam-Morogoro.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Dk. Maua Daftari, alisema inashangaza kuona bajeti ya Wizara hiyo inategemea zaidi wafadhili wa mashirika mbalimbali, hali inayotia mashaka na kuacha maswali kwamba wafadhili hao watakapokosekana Wizara itajiendeshaje.
Dk. Daftari alisema ufike wakati serikali iongeze bajeti ya Wizara ya Afya kutokana na umuhimu wake kama ilivyo kwa Wizara ya Ujenzi.
Aidha, wabunge hao walalamikia upungufu wa vitanda katika wodi za wazazi hali inayosababisha kulala wawili wawili katika kitanda kimoja.
No comments:
Post a Comment