Tuesday 9 June 2015

WAANDIKA BARUA KUOMBA KUACHA SHULE

Geita. Serikali ilianzisha mpango wa kujenga shule za sekondari za kata moja ya mikakati  ikiwa kupunguza adha ya umbali kwa wanafunzi na kusogeza huduma za elimu jirani na wananchi ili kila mtoto apate haki ya kupata elimu.

Pamoja na mpango huo kutekelezwa kwa asilimia kubwa, bado adha ya umbali wa shule kwa baadhi ya wanafunzi iko palepale, hali inayosababisha wanafunzi wengi kuacha masomo.
Shule ya Sekondari Shantamine katika Kata ya Mtakuja, Geita mjini ni miongoni mwa shule nyingi mkoani Geita  na maeneo mengi nchini ambayo bado  wanafunzi wana changamoto ya umbali wa kuifuata elimu au kurudi nyumbani.
Zaidi ya wanafunzi 27 wameacha masomo kwenye shule hiyo katika kipindi cha miezi mitano tangu kuanza kwa mwaka huu.
Taarifa zinaonyesha kuwa kati ya wanafunzi 200 walioanza kidato cha kwanza  katika shule hiyo, waliomaliza kidato cha nne mwaka jana ni wanafunzi 50.
Takwimu hizo zinamaanisha kwamba wanafunzi 150 waliacha shule huku sababu kubwa ikiainishwa kuwa ni umbali, pia mimba kwa wasichana.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisa Elimu wa Mkoa wa Geita, Eufransia Buchuma aliyoitoa mwaka 2013, wanafunzi 8,606 sawa na asilimia 50.2 kwa katika Mkoa wa Geita hawakumaliza kidato cha nne mwaka  huo kati ya wanafunzi  17,113 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2010.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo  Kakila Swillah anabainisha kwamba  tatizo hilo ni kubwa katika shule yake akieleza kuwa limesababisha wanafuzi wawili kuandika barua ya kuomba kuacha shule mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu.
“Hii inaonyesha ni jinsi gani tatizo hilo ni kubwa. Nimekuwa mwalimu mkuu katika shule nyingi, lakini sijawahi kuona mwananfunzi kwa hiari yake mwenyewe anaomba kuacha masomo kwa kigezo cha umbali. Hili ni tatizo,”anasema mwalimu huyo.
Anaeleza kuwa changamoto ya umbali imesababisha shule hiyo kuwa na matokeo yasiyoridhisha kwa wanafunzi, hasa wasichana ambapo na kwamba tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 2005,  haijawahi kutoa mwanafunzi wa kike aliyefaulu kwenda kidato cha tano na sita, bali wengi wanafeli.
Wanafunzi wanasemaje?
Zawadi Masibile (16)  na Dickson Shilinde(14) ni miongoni mwa kundi kubwa la wanafunizi walioamua kuacha shule kutokana na umbali  shuleni hapo.
Katika mahojiano na Mwananchi, wanafunzi hao wanaoishi Kijiji cha Mgusu, umbali wa kilomita 20 kutoka shuleni  wanasema kuwa walikata tamaa kutokana na kuchelewa shule kila siku huku wakitegemea kuomba lifti barabarani hivyo kuamua kuandika barua kwa mkuu wao wa shule wakieleza uamuzi wao kuacha shule.
“Kwa kweli maisha ya shule yamenishinda,sioni umuhimu wa kuendelea na masomo wakati kila siku nachelewa vipindi darasani. Kama unavyojua, huku kwetu hakuna gari kuna usafiri wa pikipiki tu unaobeba abiria kuwaleta mjini,” Masibile akionyesha kukata tamaa na kuongeza:
“Hakuna mwenye pikipiki anayekubali kunibeba mimi kunileta  shule bure, lazima nitoe pesa na wazazi wangu hawana uwezo, hivyo  kila siku natembea kwa mguu zaidi ya kilomita 20 kutoka Mgusu hadi shuleni, njia yote imejaa mapori, nikihitaji kuwahi natakiwa kuamka saa 10 usiku kila siku.”
Masibile anafafanua: “Nikichelewa shule, nafikia kwenye adhabu ya kuchapwa viboko. Iliniumiza sana hali hii, tunatukanwa na madereva wa pikipiki kila siku tukiwaomba lifti, nyumbani nafika usiku kila siku, hakuna hata raha ni karaha tu.
“Nikirudi nyumbani usiku sipati muda wa kujisomea, nafikia kwenye kazi za nyumbani, hapo unalala ukiwa umechoka na unaamka usiku wa manane kuwahi shule. Unaweza kuamka mapema, lakini ukakosa usafiri.”
Naye Shilinde anabainisha kilichokuwa kikimuuma hata kuamua kuacha shule ni kuchelewa vipindi vya asubuhi kila siku na kuambulia vipindi vya mchana tu huku akidai kwamba pia walimu hawajali kuwa wanafunzi wanatoka umbali mrefu ba kuwapa adhabu.
Anasema kwamba licha ya kutembea umbali mrefu kwenda shuleni, siku nzima inaweza kuisha wakitumikia adhabu kwa kosa la kuchelewa shule, jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma taaluma yake, hivyo kuona akiendelea kwenda shule ni sawa na kupoteza muda wake.
Siyo Masibilie na Shilinde waliokumbana na adha ya umbali, bali pia  Matokeo Kamuli, mwanafunzi wa kidato cha kwanza shuleni hapo pia ni anakabiliwa na tatizo hilo.
Anaeleza kuwa kila siku huamka saa 9:00 usiku na kuanza safari ya kwenda  shule akitumia baiskeli, lakini hufika saa 4:30  au saa 5:00 asubuhi kila siku, hivyo pia hukosa vipindi vya asubuhi na kusoma  vipindi vya mchana pekee na kwamba akitoka shule saa 9:00 alasiri  hufika nyumbani saa 4:30 usiku kila siku.
Kamuli anaeleza kuwa kijiji chao kimezungukwa na msitu uliojaa wanyama wakali hivyo kukabiliwa na hatari ya kushambuliwa na wanyama hao.
“Ikitokea baiskeli imeharibika, basi hujipa likizo hadi itakapotengemaa, ikitokea siku baiskeli haipo, hatuwezi kwenda shule kabisa kwa sababu wazazi wetu hawana uwezo wa kutupangia chumba kama walivyo wengine. Kwa kweli tunapata shida,  ukiangalia huko kwetu hakuna usafiri wa gari, yakiwepo ni ya watu binafsi au maroli ya mchanga,”alieleza.
Kwa upande wa wanafunzi wanaotoka mjini katika mkoa huo, wao kilio chao ni usafiri wakidai kwamba madereva wa  magari aina ya Hiace zinazofanya safari za mbali hukataa kuwachukua kwa kile kinachoelezwa kuwa wakiwapakia wanafunzi wanapata hasara.
“Tunaishi kwa kuomba msaada wa usafiri kwenye magari ya watu binafsi, magari ya abiria huwa hayatubebi wanafunzi  bila pesa, wazazi wetu hawatupi pesa za usafiri, hivyo siku nyingine tunajikuta tunakosa lifti hadi saa 4:00 asubuhi, hapo tunaogopa kwenda shule na unaamua kurudi,”anasema Delisi Ndigeli.
Neema John, mwanafunzi wa shule hiyo anayeishi mjini, anasema kwamba kila siku huamka saa 11:00 alfajiri ili kwenda stendi kusubiri usafiri, lakini anaweza kusubiri usafiri hadi saa 4:00 bila kupata gari, hivyo huamua kurudi nyumbani. “Ukiangalia tunakosa nafasi ya kujisomea, unaamka usiku, unarudi nyumbani usiku. Hupati nafasi ya kujisomea, hii inakatisha tamaa kwa wanafunzi, wasio na uvumilivu wanaacha shule,”anasema Neema.
Wazazi wanasemaje.
Shilinde Masanja ni baba wa mwanafunzi Dickson aliyeandika barua kuacha shule, anaeleza kuwa hapendi mtoto wake aache shule, lakini mazingira yamemsukuma akubali aache masomo.
“Mwanangu,kama unavyoniona sina uwezo wa kulipa nauli kila siku Sh4000 siwezi, hiyo ada yenyewe inanipa shida, shule wanayosoma ni mbali. Labda Serikali itusaidie usafiri kwa wanafunzi kuwe na mabasi yanayowabeba  kuwapeleka shuleni,”anasema akieleza  kuwa umaskini ndiyo sababu kuu ya wanafunzi wao kupata shida huku akiitupia lawama Serikali kwa kushindwa kujenga mabweni.
“Serikali kama iliamua kusogeza huduma za elimu kwa wananchi wake basi wafanye utaratibu shule zote  za kata ziwe na mabweni ili kuondoa usumbufu na karaha wanazopata wanafunzi,”anasema Jonas Matenge.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie anasema:”Jukumu la kuhakikisha mtoto anapata elimu bora ni la mzazi.”

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!