Rais wa Finland, Sauli Niinisto, amesema uhusiano baina ya Tanzania na Finland ni wa kudumu na utaimarishwa na kutafutiwa namna ya kuukuza zaidi ya hapa ulipo sasa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi, Premi Kibanga, Rais huyo aliyasema hayo juzi Ikulu jijini Helsinki wakati wa mazungumzo baina yake na Rais Jakaya Kikwete (pichani).
"Uhusiano wetu ni wa muda mrefu, umedumu kwa miaka 50, tumekuwa na uhusiano ambao umeleta maendeleo ya kiuchumi kwa Tanzania," alisema na kuongeza:
"Hii inatupa nafasi ya kutafuta mbinu mpya za kuleta maendeleo na kukuza ushirikiano huu zaidi,"
Rais Kikwete aliwasili Helsinki Juni Mosi, mwaka huu, kwa ziara ya kikazi ya siku tatu, ambaye pamoja na mambo mengine alimshukuru rais Niinisto kwa mwaliko wake na kumueleza hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.
Katika mazungumzo hayo, Rais pia amemueleza mwenyeji wake kuhusu uchaguzi mkuu ujao nchini Tanzania.
"Nimekuja kukushukuru pamoja na wananchi wa Finland kwa ujumla kwa mchango na misaada yenu ya maendeleo kwa Tanzania tangu nchi yetu ipate uhuru hadi leo na bado uhusiano wetu upo imara,” alifafanua.
Aidha, aliiomba Finland kuendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kukuza uchumi na kuletea watu wake maendeleo.
Pia aliwaaga na kuwashukuru viongozi na washirika wa Tanzania katika maendeleo, ambao wametoa mchango mkubwa na msaada kwa serikali na wananchi wa Tanzania katika kipindi chake cha uongozi.
Rais Kikwete pia alifanya mazungumzo na wabunge wa Finland ambao ni viongozi wa vyama vya siasa nchini humo, wakiongozwa na Spika wao Maria Lohela, na kwamba ndiye kiongozi wa kwanza kutembelea na kufanya mazungumzo na wabunge hao walioshika nyadhifa hizo Aprili, mwaka huu.
Rais Kikwete pamoja na mambo mengine, ametembelea chuo Kikuu cha Aalto jijini Helsinki ambacho ni chuo cha tatu kwa ukubwa nchini Finland, pia chuo hicho kina utaratibu wa kubadilishana wanafunzi na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)
No comments:
Post a Comment