Na Masanja Mabula -Pemba .
……………………………………….
Mkuu wa Wilaya ya Wete Hassan Khatib Hassan amesema kuwa tabia za baadhi ya askari wa jeshi la Polisi za kutotunza siri kutoka kwa wananchi kunakwamisha ufanisi wa mapambano dhidi ya udhibiti wa madawa za kulevya .
Amesema kuwa ili kufanikisha azma ya kukabiliana na waingizaji , wasambazaji pamoja na watumiaji wa dawa za kulevya ni budi Jeshi la Polisi Wilayani humo kuwachukulia hatua askari ambao wanatoa siri wanazopelekea na wananchi .
Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua mkutano wa siku moja uliowashirikisha Masheha , watendaji wa Piolisi la Wilaya pamoja na watendaji kutoka Idara ya kuratibu na kudhibiti dawa za kulevya zanzibar uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Mifugo Pemba .
“Tabia za baadhi ya askari za kutotunza siri wanazopewa na wananchi kunakwamisha vita dhidi ya waingizaji na wasambazaji wa dawa za kulevya , hivyo wanatakiwa kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ” alifahamisha .
Mkuu huyo wa Wilaya amekiri kwamba ni vigumu kuweza kuidhibiti biashara hiyo kutokana na kwamba hakuna anayekifahamu kiwanda kinachozalisha dawa hizo na kuongeza kwamba kama kiwanda kingefahamika kingefutiwa leseni .
“Ugumu wa mapambano hayo unakuja kwani hakuna anayekifahamu kiwanda kinachozalisha dawa hizi na kama kingefahamika ingekuwa rahisi kufuta leseni yake , lakini kilicho mbele yetu ni kukabiliana na waatumiaji wa dawa hizi ” alisisitiza .
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amefahamisha kwamba kukosekana kwa mahusiano na ushirikiano kwa taasisi za Serikali na binafsi pia ni sababu inayosababisha wahusika wa dawa za kulevya kutotiwa hatiani .
Kwa upande wake Mkuu wa jeshi la Polisi Wilaya ya Wete Omar Othuman amesema kuwa vitendo vya kutotunza siri zinasababishwa na baadhi ya askari ambao sio waaminifu na ambao wamekaa katika kituo kimoja cha kazi kwa zaidi ya miaka kumi .
Hata hivyo amewataka wananchi ambao wanatoa taarifa na kisha siri kuwafikia watuhumiwa kuwaripoti katika Ofisi yake kwa ajili ya kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria kwani wanalipaka matope jeshi zima .
“Wapo baadhi ya askari wamekaa katika kituo kimoja cha kazi kwa zaidi ya miaka kumi na hivhyi kujenga mazoea , hivyo nawaomba wananchi waleteni majina yao ili tuwachukuliwa hatua za kinidhamu ” alisema OCD .
Mapema akizungumza kwenye mkutano Mkurugenzi wa Idara hiyo Heriyangu Mgeni Khamis amesema kuwa kutokana na kushamiri kwa vitendo vya utumiaji wa dawa za kulevya kumepelekea ongezeko na watoto wenye matatizo ya akili .
Hata hivyo baadhi ya masheha wamesema kuwa bado vyombo vya sheria havijajipanga kukabiliana na matendo hayo kwani wahusika wanaokamatwa hawachukuliwi hatua .
Sheha wa Mtemani Wete Mrisho Juma Mtwana (Magogo) amesema kuwa kumweka nje kwa dhamana mtuhumia wa dawa za kulevya kunamfanya aendelee na biashara hiyo huku pia akisema upelelezi wa mashauri hayo unachelewa kukamilika .
Kikao hicho ni kauli shamra shamra na siku ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya duniani ambapo ujumbe wake kwa mwaka huu ni imarisha afya yako achana na utumiaji wa dawa za kulevya .
No comments:
Post a Comment