Sunday, 7 June 2015

NAWAPENDA MAKAHABA!



Unashangaa nini? Ndiyo nawapenda tena kwa dhati na wala sioni aibu kusema hivyo, kwani nao ni binadamu kama mimi na wewe, na kama wana makosa hata wewe unayo makosa yako; na pengine makosa yako ni mabaya zaidi yenye athari kubwa kwa wanajamii na taifa pia. Naomba nieleweke vyema kwamba sitetei ‘ukahaba au vitendo vya umalaya’ na wala sipendi viendelee kuwepo bali nasononeshwa na jinsi wanavyotendewa!

Ndani ya kitabu kitakatifu cha Biblia imeandikwa na hii ni amri ya Mwenyezi Mungu wala siyo ombi ya kuwa: “…waheshimu baba yako na mama yako, na mpende jirani yako kama nafsi yako. Soma Mathayo 19:19. Ni jirani, watoto na wenzetu wenye shida kama wewe.
Kahaba ni nani
Kamusi ya Kiswahili Sanifu inaeleza ya kuwa Kahaba ni: “…mtu mwanamume au mwanamke anayeshiriki mambo ya uasherati kuwa ni biashara au starehe yake; malaya, mzinifu, mzinzi”. Yawezekana mimi si-mjuzi wa sheria zinayowahusu makahaba, lakini naamini shitaka la ukahaba linahitaji ushahidi makini la utendwaji wake zaidi ya kumkamata mwanamke akiwa baa na amekaa mezani na kinywaji chake peke yake; hapo hajawa kahaba!
Naamini kabisa watendaji wanaowakamata hao waitwao makahaba wakitekeleza sawa sawa amri za Mwenyezi Mungu kwa upendo hawatalazimika kutumia nguvu za kupita kiasi tunazoziona zikitumiwa na baadhi ya askari wetu, nyakati za usiku kwani huwaburuza kwa nguvu mno, kuwapiga mabuti na wengi wao wakiwa ni wasichana wadogo wasio na nguvu kabisa.
Unapoliona sakata hilo kweli utawaonea huruma, sisemi askari wasifanye kazi yao waliotumwa, bali utendwaji wake ni wa kuzidi kiwango cha mateso hata kabla hawajafikishwa kwa Pilato. Ni watoto wetu, ni jirani zetu ni wanajamii wenzetu, pia serikali wajiulize maswali kadhaa yenye majibu makini yatakayoleta ufanisi wa kuiondoa kadhia hii ya ukahaba au kuipunguza kwa kiasi kitakachoridhisha kwani yote hayo tukubali ni tatizo linalohusu wanajamii na watawala kwa ujumla.
Baa ni wanaume tu
Wanapotenda kazi hiyo kwa kweli kabisa tunashuhudia wakiwa na hasira-nao, wakali, wenye lugha za kukebehi, kutusi na kuwanyanyasa kupita kiasi na yote haya hayafanyiki kwa kificho ni wazi kabisa tena mbele ya wateja wengine kwenye hizo baa. Wanajamii na Serikali tujiulize je! mabinti zetu wanapenda kuwa malaya? Ni nini chanzo cha yote haya? Mabinti hao huwa hawapewi nafasi yoyote ya kujitetea kwa nini wako baa, ili mradi wamekutwa baa usiku basi wote ni malaya.
Tujiulize, je, wasichana wanatakiwa kustarehe baa kuanzia saa ngapi hadi saa ngapi na hasa baa hizo zikiwa na vibali vya ‘night club’? pindi mwanaume anapojaribu kutoa utetezi kuwa huyu ni rafiki yangu; ghafla anageuziwa kibao na kuambiwa ‘unatuzuia kufanya kazi yetu’ – naye anashikwa ghafla anapata kipigo kama jambazi hali hii huwaletea adha baadhi ya wanaume waliofuatana na wapenzi wao na hata wake zao. Si kila mwanamke anayekwenda baa anajiuza mwili wake. Je, ipo sheria inayosema kuwa ni lazima mwanamke au msichana afuatane na mwanaume baa wakati wa usiku? Wale wasichana wanaojiuza miili yao kando kando za barabara hao kwa kweli wakamatwe. Ni Aibu tupu!
Umalaya au uzurulaji
Je, polisi wanapofika kwenye baa na kuwakusanya wanawake hao wana kigezo gani cha huo umalaya. Na je, huyo malaya atakuwaje amekamilika umalaya wake bila ya mwanaume malaya? Wasichana hao wanaoitwa makahaba wanapofikishwa mahakamani wengi wao wanafunguliwa kesi za uzururaji na ati pia kwa kuwa hawana vitambulisho vya kazi; mbona wapiga debe hawakamatwi na hawana vitambulisho. Na wanaume walioko baa nao pia ni wazurulaji? tena wala hawauliziwi vitambulisho vya kazi. Hao wasichana wanapohukumiwa kwenda jela au kulipishwa faini, Je, kwa njia hiyo ndiyo Watawala wamelitatua kabisa tatizo hili la ukahaba au umalaya?
Ni kwa kiwango gani ambacho Wizara-husika ya serikali imefanya bidii inayotambulika; kwa mfano kuwaita kwa vikundi au kuwatembelea maeneo wanayoishi na kuwapa ushauri nasaha-yaani kuwanasii jinsi gani wanavyoweza kuepukana na biashara hiyo hatari na haramu yenye kujidhalilisha utu wao; pia wanavyoweza kuwa wajasiriamali na kuwawezesha kwa mikopo nafuu ya vikundi? Wizara ya Wanawake, Jinsia na Watoto wanayo bajeti ya kila mwaka kwa wahusika hawa, iweje iwasahau kabisa?
Nashauri tusijenge wigo wa uadui na chuki kati ya watawala ama polisi na wanawake/wasichana hawa wanaoponzwa na umasikini wao na kukutwa katika majumba ya starehe ambayo ni haki yao kuwepo hapo, utumiwe utaratibu mzuri wenye busara, usiodhalilisha utu wao na uwe ni mkakati wa kudumu kwa maendeleo ya mabinti zetu hao.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!