Thursday, 11 June 2015

MKULIMA ANOGESHA MBIO ZA URAIS

MKULIMA kutoka Kasulu mkoani Kigoma, Eldeforce Bilohe (43) jana alichukua fomu za kuwania urais na kusema kuwa kati ya wagombea 27 ambao wamejitokeza haoni kama kuna mgombea ambaye ni tishio kwake.

“Kati ya wagombea 27 ambao tayari wamechukua fomu kabla yangu sioni kama kuna mgombea tishio kwangu,” alisema mgombea huyo huku akishangiliwa.
Bilohe alifika ofisi za makao makuu ya CCM saa nane mchana ambapo alilakiwa kwa shangwe na vigelegele na watumishi wa CCM makao makuu.
Hata hivyo, alishindwa kueleza vipaumbele vyake mpaka anamaliza muda wa kujieleza. Mgombea huyo ambaye alisahau kuzima simu yake wakati akizungumza simu hiyo ikaita na kuamua kuipokea.
“Subiri kidogo,” aliongea na simu kisha akakata. Akizungumza juu ya azma yake, alisema ameamua kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani amekuwa na dhamira hiyo tangu mwaka 2003.
“Dhamira hiyo iko moyoni tangu mwaka 2003 pale ambapo nilipotaka kuweka mambo sawa baadhi ya mambo yalijitokeza na kuchelewesha kusudio hilo,” alisema.
Alisema ilipofika mwaka 2015 aliamua kurudia nia yake ya dhati na Februari 5, mwaka huu alitangaza azma hiyo kwenye gazeti ya Sauti Huru. “Ninaomba kutafutiwa wadhamini kila mkoa ili kusaidiana nani kufika Dodoma kuomba kuteuliwa na CCM.”
Alisema kabla ya kuchukua uamuzi huo aliuliza baadhi ya watu ambao baadaye walimshauri agombee nafasi hiyo. “Nikafuata utaratibu baadae wakaniambia nikagombea, nikaenda kwa mwenyekiti akaniuliza je utaweza, nikamjibu nitaweza nikamwambia cha msingi ni kuniweka kwenye sala,” alisema.
Alisema wakati akijiandaa kufika Dodoma likajitokeza suala la kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ikabidi amalize zoezi hilo.
“Ilipofika Juni 3, mwaka huu nikawaomba barua ya kwenda Dodoma wakalifanyia kazi suala hilo, nikafika CCM mkoa wakakubali.” Alisema elimu yake ni ya taifa (darasa la saba) na amefika Dodoma kuchukua fomu za kugombea Urais akiwa kama Mtanzania “Nimekuja kama Mtanzania sikuja kama mchezo wa kupoteza fedha zangu”.
Alisema fedha za kuchukua fomu zimetoka mfukoni mwake na hajachangiwa na yeyote. Alipoulizwa kwa nini hajaongozana na mkewe alisema kwa sababu ambazo hazijaweza kuzuilika, mkewe alimtaka atangulie lakini pale atakapohitajika atapatikana.
Alipohojiwa kwa nini hana vipaumbele kutokana na nafasi anayogombea kuwa ni nyeti alisema ajira kwa vijana na maisha bora kwa wastaafu.
Juzi mgombea huyo alitinga makao makuu ya CCM kuchukua fomu ya kuomba ridhaa kuteuliwa kuwa mgombea bila kuwa na ada, jambo ambalo lilifanya zoezi lake la kuchukua fomu kuahirishwa.
Mjasiriamali naye ajitosa Mkazi wa Kata ya Mwisenge Wilaya ya Musoma mkoani Mara, Boniface Ndengo (40), jana alichukua fomu ya kuwania Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema ameamua kuchukua fomu ili kutimiza azma yake ya kutumikia wananchi. Ndengo ambaye mtaalamu wa masuala ya biashara na uongozi, alisema watu wanafanya siasa kama mambo ya kubahatisha bahatisha tu, lakini siasa ni taaluma inayoshughulika na kuboresha maisha ya watu na ana majukummu makubwa ya kushughulikia.
Pia alisema amekuwa akishangazwa kuona watu wenye umri mkubwa wakitafuta madaraka makubwa ya kutumikia wananchi wakati wakiwa wamechoka.
Alisema mtu anapofikia umri wa kustaafu anatakiwa kupunzika na si kutafuta kufanya shughuli za kisiasa. Alisema uongozi unatakiwa kufanywa na watu wenye umri wenye nguvu na si wenye umri wa kustaafu.
“Ni jambo la kujiuliza kwa nini kazi ya Urais inatafutwa na watu wenye umri wa kustaafu kwani umri wao umeshakuwa mkubwa na watu wameshachoka na wanatakiwa kupumzika,” alisema.
Alisema mahitaji makubwa ya Watanzania ni kupata kiongozi wa nchi atakayeweza kuondokana na umaskini. Alisema akiwa kama mtaalamu wa masuala ya biashara na uongozi na moja wa wahitimu wenye ufaulu bora kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amekuwa mbunifu wa mifumo mbalimbali ya kufaulisha sekta binafsi.
Alisema kutokana na taaluma hizo ameona ni wakati muafaka kwake kuwashawishi Watanzania kumpa fursa kutekeleza jukumu kubwa la nchi ilikusaidia watanzania kutoka kwenye umaskini.

1 comment:

Anonymous said...

aziz bilal18:57


1


Sawa,hiyo ni habari njema kwa upinzani,leteni yeyote yule lakini safari hii kitaeleweka tu.

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!