Kuongezeka kwa migogoro ya ardhi nchini inatokana na baadhi ya wataalam wa uthamini na usimamizi wa majengo kutozingatia maadili katika utendaji wao wa kazi.
Hayo yameelezwa jijini Dar es salaam jana na Mhadhiri wa Shule kuu ya Uthamini wa mali na Usimamizi wa fedha (SRES), Banjuni Maulid, wakati wa maadhimisho ya siku ya shule hiyo.
Maulidi alisema kama hali hiyo haitadhibitiwa haraka itaweza kuleta mpasuko ndani ya jamii kutokana na watu wengu kudhulumiwa haki zao.
Kwenye maadhimisho hayo wazazi, walimu, wadau na wanafunzi walikutana kwa ajili ya kujadili namna fursa za uendelezaji wa ardhi na usimamizi wa fedha unavyoweza kuchangia upatikanaji wa ajira kwa wanaohitimu shuleni hapo.
Alisema wataalamu hao kwa sasa wameacha kufuata maadili kwa mujibu wa fani zao, badala yake wameweka mbele maslahi binafsi kwa kuongeza au kupunguza thamani ya mali kulingana na matakwa yake.
“Tumeshuhudia jinsi baadhi ya maafisa wathamini wanaongea na wamiliki wa mali ili waongeze thamani ya fidia kwa ahadi ya kupewa sehemu ya pesa, jambo hili ni kinyume na maadili na ndio chanzo cha kuendelea migogoro ya ardhi nchini,” alisema Maulid.
Aliwataka wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo kuwa sehemu ya wataalam watakaopunguza tatizo hilo kwa kufanya kazi kwa weledi.
Alisema shule hiyo ambayo ipo chini ya Chuo Kikuu cha Ardhi (UCLAS) imefanikiwa kufundisha masomo ya uthamini wa mali, usimamizi na uangalizi wa majengo pamoja na usimamizi wa fedha unaotambulika kimataifa.
Awali mgeni rasmi Meneja wa Association of Chartered Accountants, Genard lazaro, alisema kwa kutumia mkusanyiko huo wanafunzi wamepata nafasi ya kuona fursa za ajira kupitia kwa wadau walioshiriki.
Aliwataka wanafunzi kuacha kuweka akili zao katika kuajiriwa mara watakapomaliza, badala yake wabuni njia za kujiajiri kulingana na nafasi zao.
Mwanafunzi wa shule hiyo, Masanja Ezekiel, alishukuru kupata nafasi hiyo ya kukutana na wadau mbalimbali, ambapo alisema imekuwa na nguvu ya mpya na kujiona anaweza kupata mafanikio mara atakapomaliza masomo yake.
Alisema wakati wa wanafunzi kusoma kwa ajili ya kuajiriwa imepitwa na wakati, hivyo waweke kipaumbele kwa kutafuta fursa za kujiajiri.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment