Akizungumza na BIN ZUBEIRY kutoka Ujerumani leo, beki huyo wa kushoto amesema kwamba amesaini klabu hiyo baada ya kufuzu majaribio wiki mbili zilizopita.
“Sikutaka kusaini Mkataba wa muda mrefu, kwa sababu malengo yangu ni kufika mbali. Nataka niitumie timu hii ili nionekane niende ligi za juu,”amesema.
Mgeta ambaye Okotba 10 mwaka huu atatimiza miaka 21, amesema kwamba kwa mara ya kwanza alikwenda Ujerumani mwaka 2012 wakati huo bado mchezaji wa akademi ya TSC ya Mwanza.
“Tulikuwa wachezaji 22 chini ya kocha Rogasian Kaijage, tukacheza mashindano ya vijana ambayo yalishirikisha timu nyingi za nchi nyingine,”amesema.
Anasema baada ya mashindano hayo, Macabi Haifa ya Israel ilivutiwa naye na kuanza mipango ya kutaka kumchukua, lakini akashindwa kubaki kwa sababu wakati huo alikuwa kwenye kikosi cha timu ya vijana ya taifa chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes.
Emil Mgeta akifurahia baada ya kusaini Mkataba na Neckarsulmer Sports Union ya Ligi Daraja la Nne Ujerumani jana
“Yule Mjerumani Jugern Seitz aliyetupeleka kule Ujerumani, ndiye alikuwa anashughulikia ile dili, na nikiwa kambini na Ngorongoro tuliendelea kuwasiliaja, ila baada ya mechi za kufuzu Fainali za Afrika tulipotolewa, ikatokea sintofahamu na ile dili ya Macabi Haifa ikafa,”anasema.
Kufuatia kufa kwa dili hilo, Mgeta anasema kwamba akajiunga na timu ya vijana ya Simba SC, maarufu kama Simba B kwa mkopo kutoka TSC.
Hata hivyo, anasema Seitz alikuja tena Tanzania mwaka 2013 na akawachukua yeye wachezaji wengine tisa wa Simba B, wakiwemo Said Ndemla na Frank Sekule kwenda tena Ujerumani.
“Ilikuwa Mei mwaka 2013 sisi tulitokea kambi ya timu ya pili ya taifa (Young Taifa Stars) tukaenda Ujerumani hadi mwezi wa saba tukarudi. Niliporudi Mkataba wangu ukawa umekwsiha TSC, nikasaini Mkataba wa miaka mitatu na Simba SC,”anasema.
Hata hivyo, Mgeta anasema mambo yake yakawa magumu Simba SC baada ya ujio wa kocha Mcroatia, Zdravko Logarusic na hatimaye mwaka jana akaandika barua ya kuvunja Mkataba.
Emile Josiah Mgeta akipita katika mitaa ya Ujerumani
“Wakati wote nikiwa Simba SC kuna mtu kule Ujerumani alivutiwa na mimi na tukawa tunawasiliana. Sasa nilipomuambia nimevunja Mkataba na klabu yangu, akaanza kunifanyia mipango ya kupata timu kule. Mambo yameenda hadi alipofanikiwa nikaondoka na kuja huku tena, hatimaye jana nimesaini Mkataba,”amesema.
Emil Josiah Mgeta alimpoteza baba yake mzazi akiwa bado kichanga wa miezi sita na amelelewa na mama yake tu, Editha wilayani Ukerewe alikozaliwa na kukulia.
Elimu ya msingi amepata katika shule ya Kagera na sekondari Bukongo zote za Ukerewe hadi Kidato cha Nne.
Akiwa Kidato cha Pili tu, tayari alianza kuchezea UDC ya Ukerewe na alipomaliza Kidato cha Nne akaenda kujiunga na TSC, baadaye Simba SC. Amecheza U20 na Young Taifa Stars na ni kati ya wachezaji ambao miaka miwili iliyopita walitabiriwa kuwa nyota wa taifa baadaye. Kila la heri Emil Josiah Mgeta.
credit.bin Zubeiry
No comments:
Post a Comment