Thursday, 4 June 2015

MAREKANI TANZANIA KUSHIRIKIANA KUIMARISHA SEKTA YA NISHATI


Serikali ya Marekani imesema itaendeleza mahusiano baina yake na Tanzania katika sekta ya nishati ili kukuza uchumi na kujenga miundombinu endelevu katika sekta hiyo.

Katibu Msaidizi wa Nishati na Mafuta wa Marekani kutoka Idara ya Nishati, Christopher Smith, aliyasema hayo jana mara baada ya kutembelea mtambo wa kufua umeme wa Kinyerezi unaodhaminiwa na Marekani kupitia mradi wa MCC.
Alisema serikali za Marekani na Tanzania zitaendelea kushirikiana katika masuala ya nishati ili kufikia malengo waliyopanga ya kuhakikisha tatizo la ukosefu wa umeme kwa wananchi linamalizika.
Alisema mradi wa ujenzi wa vinu vya kusambaza umeme wa Kinyerezi vitatumia gesi utakapomalizika kutasaidia kwa asilimia kubwa kusambaza umeme kwa wananchi.
Naye Meneja Miradi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Simon Jilima, alisema ujenzi wa mradi huo wa uzalishaji umeme kwa sasa umefikia asilimia 88.
Alisema hatua inayoendelea kwa sasa ni kuunganisha nyaya katika gridi ya taifa na nguzo zimeshawekwa ili majaribio yatakapoanza ya kuwasha mtambo huo umeme uweze kuingia moja kwa moja.
Alisema majaribio ya kuwasha mtambo huo yataanza Julai, mwaka huu, lakini kutakuwapo na majaribio ya awali yatakayoanza mwishoni mwa mwezi huu.
“Umeme utaanza kuingizwa katika gridi ya taifa mwezi ujao, lakini ni lazima kuwa na majaribio na siyo kuwasha moja kwa moja hivyo majaribio yataanza mwishoni mwa mwezi huu,” alisema Jilima.
Alisema majaribio hayo yatafanyika katika mitambo na katika njia za kupitishia umeme na yanaweza kudumu kwa kipindi cha mwezi mmoja na kwa wakati wa kufanya majaribio hayo uzalishaji utakuwa unaendelea.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!