1.Miliki furaha yako wewe mwenyewe
Ni vyema ukifahamu kwamba baadhi ya vitu unavyovitegemea vinaweza visikupe furaha unayoitamani, yamkini mumeo au mkeo asikupe furaha, yamkini fedha na mali ulizonazo zisikupe furaha ya kweli. Jaribu kubeba jukumu la kujihakikishia una furaha pasipo kutegemea mazingira ya vitu au watu wanaokuzunguka. Chukua jukumu la la kuzalisha, kuitunza na kuiendeleza ile furaha na amani inayoishi ndani yako.
2. Badilisha namna
unavyoongea kuhusu wewe mwenyewe
Upo uwezekano mkubwa kwamba maisha yako na historia yako ya nyuma haitabiri kabisa mafanikio na furaha yako ya sasa na ya baadae. Jifunze na jitahidi kwenda kinyume na historia yako, tena ikiwezekana tengeneza mazingira ya kuikanusha historia hiyo yenye harufu ya kushindwa. Badili namna unavyojiongelesha mwenyewe na pia vile unavyoongea kuhusu wewe. Fahamu kwamba katika kule kuzungumza kwako unajiandikia mwongozo “script” ya maisha yako, ukijizungumzia vema basi inajitengenezea mwongozo wa furaha na mafanikio, ukijizungumzia vibaya vivyo hivyo unajiandalia “script” ya kushindwa na kutofanikia maishani.
3. Jifunze kuifurahia safari ya maisha yako
Maisha ni mchakato na sio mustakabali, hata kama upo mustakabali au mahali tunatamani kufika huko mbeleni ni lazima tuiheshimu na kuifurahia safari ya kufikia kule. Usikae kila siku ukisema nitajipa furaha nikifikia hapa au nikifikia pale, nita furahia maisha nikishaolewa, au nikisha maliza digrii, au nikisha nunua gari au nikisha jenga nyumba. Watoto wangu watafurahia maisha na mimi tukisha hamia kwetu, au wakisha kuwa wakubwa. Kwani nani ana uhakika wa kufika huko anapopatamania? Furaha ya huko unakoelekea inategemezwa sana na jinsi unavyofurahia safari ya kuelekea huko. Jifunze kufurahia kila mafanikio unayoyapata hata kama ni mafanikio madogo. Kama hauwezi kuyafurahia mafanikio madogo uliyonayo je utawezaje kuyafurahia mafanikio makubwa?. Kama hauto furahi na kumshukuru mungu wewe na ndugu zako na familia yako kwa kupata stashahada, je utaweza kufanya kasherehe ukipata shahada au zaidi ya shahada? Kufurahia kila hatua hutupa kiu na hamasa katika kujipanga kwa hatua nyingine kubwa zilizopo mbele yetu. Usiicheleweshe furaha yako, furahia safari nzima na sio kuikusanya au kuilimbikiza furaha yako eti utafurahia huko mbeleni. Kama usipojionyesha kwamba wewe ni wa thamani na unathamani basi fahamu kuwa hakuna atakaye kuheshimu. Njia mojawapo ya kujionyesha uthamani wako ni kufurahia kila chema kinachotokea kwenye maisha yako
4.Boresha uhusiano wako
Kila kitu maishani ni kuhusu uhusiano, kila kitu maishani kinaweza kuyaathiri mahusiano yako, ama vizuri au vibaya. Hakikisha mahusiano yako na Muumba wako yamekaa sawa na unayafurahia. Kama hauna furaha kutokana na mahusiano yako na Mungu basi kuna uwezekano maeneo mengine yote yakakosa furaha. Jambo la pili, hakikisha mahusiano yako na wewe mwenyewe yako sawa na tena uyafurahie wewe mwenyewe.
Unapoyafurahia mahusiano uliyonayo baina yaw ewe mwenyewe unawanyima nafasi ya kuisumbua furaha yako wale wanaojabu kucheza na furaha yako, na mtu yeyote hawezi kujidai kwamba yeye ndiyo sababu ya furaha yako.
Kuna uwezekano mkubwa kwamba kila anayeingia kwenye maisha yako akifikiri kwamba anakuletea furaha anakukuta tayari uko kwenye sherehe ya kuyafurahia maisha yako na hii inaweza kuwafanya na wao kuendeleza furaha zao.
Hapa unakuwa chachu nzuri kwa. Pia boresha mahusiano yako na mwenza wako, watoto wako, ndugu zako, marafiki zako. Kimsingi hauwezi kuzaa matunda kama mahusiano yako sio mazuri, ama iwe kwenye kazi, biashara, elimu, familia au hata katika imani, mafanikio yako yanategemea sana mahusiano uliyonayo na wengine.
5. Weka uwiano mzuri katika maisha yako
Maisha yana shinikizo kubwa sana kama hauwezi kuweka uwiano mzuri katika maisha yako ya kila siku. Najua tunafanya kazi na tunaheshimu kazi zetu lakini yako maisha mengine nje ya kazi, kazi sio kila kitu maishani kwetu, tuna familia zetu zinatuhitaji sana, wake, waume na watoto wetu, tuna imani, inatubidi kuzipamuda pia katika maeneo ya ibada, tuna ndugu na marafiki.
Miili na akili zetu pia zinahitaji utulivu binafsi na sisi wenyewe tunahitaji muda wetu binafsi. Hata farasi wa vita hupata muda wa kupumzika. Siyo lazima kila wakati uonekane mkakamavu kwa ajili ya kazi, au kila wakati wewe na mavazi ya kazini, lini watoto wako watakuona na mavazi ya michezo?
Lini wafanyakazi wenzako watakuona ukiwa nje ya suti ukishiriki nao michezo? Lini watu watajua vipawa au vipaji ulivyonayo? Mfano kuimba, kucheza, kuchora, nk. Ukikomaa na kitu kimoja tu maishani unaweza ukafa kabla ya muda wako. Usifikiri kujichanganya na jamii ni ushamba na ni kukosa kazi ya kufanya.
Imeandaliwa na Dk Chris Mauki.Baruapepe: chrismauki57@gmail.com
www.chrismauki.com
No comments:
Post a Comment